Munich wanawakaribisha leo mabingwa Wolfsburg | Michezo | DW | 28.08.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Munich wanawakaribisha leo mabingwa Wolfsburg

Nani atatamba Allianz Arena ?

default

Trainer Louis van Gaal wa B.Munich mashakani ?

-Mabingwa wa Bundesliga-Wolfsburg, wana miadi jioni hii na Bayern Munich ambayo haikushinda tangu kuanza msimu mpya.Nini hatima ya kocha wa Munich -mdachi van Gaal ?

-Kura imepigwa ya jinsi madume wa Champions League watakavyoumana -Bayern Munich wakiwa kundi moja na Juventus ya Itali wakati mabingwa Wolfsburg wameangukia kundi moja na Manchester united.

-Kocha wa Ujerumani Joachim Loew,atangaza kikosi chake kitakacho pambana na Bafana Bafana-Afrika kusini wiki ijayo mjini Leverkusen.

-Na mzee Nelson Mandela, ampongeza bingwa wa dunia wa mita 800 Caster Semenya anaetiliwa shaka si mwanamke.

Mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani-Bayern Munich, lazima watambe nyumbani jioni hii (Jumamosi) mbele ya mabingwa Wolfsburg ama sivyo,msiba uliowapata mapambano 3 yaliopita wa kutoshinda, utazusha balaa kubwa zaidi mjini Munich.Kocha wao mpya mdachi Van Gaal, kiti chake kitatikisika zaidi na vilio vya kumtimua na mapema vitaongezeka. Bayern Munich utakumbuka, ilizabwa mabao 2-1 na chipukizi waliopanda daraja ya kwanza msimu huu Mainz. Munich lakini, kabla ya firimbi kulia jioni hii ,ilijiimarisha kwa kumuajiri Arjen Robben kutoka Real Madrid - Spain.

Taarifa zasema kwamba, Munich imelipa kitita cha Euro milioni 25 kumkomboa wingi Arjen Robben ambae hahitajiki wakati huu katika kikosi cha Real kutokana na kuwasili huko kwa mreno Cristiano Ronaldo.Real ililipa kitita cha Euro milioni 35 kwa Chelsea kumkomboa Robben hapo 2007.

Kwahivyo, Bayern Munichambayo katika kura ya champions-league -kombe la klabu bingwa barani ulaya imeangukia kundi moja na Juventus, inatapatapa leo kushinda Allianz Arena ili kujiokoka kutoka mwanzo mabaya kabisa wa msimu tangu kupita miaka 43. Kocha wao wa zamani na sasa anaeiongoza Schalke,Felix Magath alidai majuzi kwamba timu nyengine katika Bundesliga zimeshapoteza heshim zao kwa Bayern munich na haziigopi tena.Msimu uliopita hata Fc Cologne,inayoburura mkia wa Ligi wakati huu iliondoka na pointi 3 mjini Munich.

Mabingwa Wolfsburg ambao wameangukia kundi moja na Manchester united katika champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya, waliteleza kwa mara ya kwanza nyunmbani mwishoni mwa wiki iliopita walipopokonywa pointi 3 na Hamburg.Kwa mara 20 Wolfsburg, ilikuwa haikushindwa nyumbani.

Hamburg jioni hii imeikaribisha FC Cologne ambayo pia kama Bayern Munich, imeanza vibaya msimu huu ikiwa na pointi 1 tu hadi sasa.Leverkusen inayoongoza Ligi wakati huu wanaikabili Bochum na Schalke wanacheza na timu ya mkiani Freiburg.

Stuttgart ambayo hivi punde tu imekata tiketi yake ya kombe la ulaya la champions-league, ina miadi nyumbani na Nuremberg.Borussia Dortmund yataembelewa na Eintrach Frankfurt.Hannover inakamilisha kalenda ya mwishoni mwa wiki hii kwa changamoto na Hoffenheim.Kesho Jumapili itakuwa zamu ya Berlin kuoneshana na Bremen kile klichomtoa kanga manyoya.

Kocha wa Ujerumani, Joachim Loew ametangaza kikosi chake kitakachopambana na Bafana Bafana -Afrika Kusini jumamosi ijayo mjini Leverkusen.Loew amewaacha nje ya kikosi hicho mastadi 2 wa Werder Bremen, Torsten Frings na kipa Tim Wiese.Pia hawatakuwamo katika mpambano ujao wa kuania tiketi ya kombe lijalo la dunia dhidi ya Azerbaijan mjini Hannover Septemba 9.

Kipa wiese alievaa jazi ya Taifa kwa mara ya kwanza pale Ujerumani ilipocheza na Uingereza na kushinda 2-1 mjini Berlin ,Novemba mwaka jana, anajikuta sasa nafasi ya 4 ya orodha wa makipa wa Ujerumani akija nyuma ya kipa wa Leverkusen, Rene Adler na wa Schalke ,Manuel Neuer.Kocha Loew anajiandaa kwa changamoto kali hapo Oktoba na Russia itakayoamua ipi kati yao, itaondoka na tiketi ya Kombe la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.

Mashindano makali zaidi yapo katika kikosi cha washambulizi akina Cacau wa Stuttgart,mbrazil aliechukua uraia wa Ujerumani na Lukas Podolski wa FC Cologne,Mario Gomez na Miroslav Klose wa Bayern Munich.

Kocha wa Nigeria Shuaibu Amodu, amemkasirikia mno stadi wa mabingwa wa Ujerumani Wolfsburg, Obafemi Martins kwa tabia yake anayodai haipendezi. Kwahivyo, kocha Amodu ameamua kumtoa nje ya kikosi cha Nigeria kwa mpambano wa mwezi ujao wa kombe la dunia dhidi ya Tunisia,mjini Abuja.

Kocha Amodu amedai alishindwa kuwasiliana na Martins anaecheza dimba katika Bundesliga kabla ya ziara yake ya ulaya hivi karibuni.Mwishoe, lakini kocha wa Nigeria aliweza kuwasiliana na stadi huyo wa zamani wa New Castle wiki iliopita .Martins alimuarifu kwamba yutayari kucheza katika mechi hiyo na Tunisia.

Nigeria inapambana na tunisia jumapili ijayo katika mechi ya kufa-kupona .Obafemi anaetamba katika klabu bingwa ya Ujerumani Wolfsburg, ameshatia mabao 2 katika kila mechi 2 alizocheza. Nigeria, ilikosa kucheza pia katika Kombe lililopita la dunia ilipotolewa nje na Angola.

Kura ilipigwa mwishoni mwa wiki hii kuamua msimu mpya wa champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya:Kundi A linajumuisha Bayern munich ya ujerumani, Juventus Turin ya Itali, Bourdeaux ya Ufaransa.

KUndi B,linaingiza mabingwa wa Ujerumani :Wolfsburg; Manchester united ya uingereza, ZSKA Moscow na Basiktas Istanbul.Kundi C linaingiza AC Milan ya itali,Real Madrid ya Spian,Olympique Marseille ya Ufaransa na FC Zurich.Kundi D kuna chelsea ya Uingereza, FC porto ya Ureno,Athletico Madrid ya Spain na Nikosea ya Cyprus.

Liverpool ya Uingereza imeangukia kundi E pamoja na wafaransa Olympique Lyon,AC Florenz yaItali na Bebrecen.Majogoo wa FC Barcelona nchini Spain, watakuwa na miadi na Inter Milan ya Itali,Dynamo Kiev ya Ukrain na Rubin Kasan ya Urusi.

Stutgart ya Ujerumani iko kundi G pamoja na FC Sevilla ya Spain ,Glasgow Rangers ya Scotland na Urziceni (Uzicheni) ya Rumania .Kundi la mwisho H, linakamilishwa na Arsenal ya uingereza ,Alkamaar ya holland,Olympiakos ya ugiriki na Standard Luttich ya Ubelgiji.Mashabiki wa champions League wanasubiri kwa hamu firimbi kulia.

Tumalizie kisa kilichogonga vichwa vya habari wiki hii:Kurejea nyumbani Afrika kusini kwa bingwa wa mita 800 wanawake au je, wanaume ? Hilo ndilo swali linalolitaabisha shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF.Kwa waafrika kusini lakini, ni wazi kabisa kwamba bingwa wao Caster Semenya ni mwanamke. Ili kutilia nguvu dai hilo, Semenya alikaribishwa kwa shangwe na shamra shamra uwanja wa ndege wa Johannesberg alipowasili hapo Jumaane.

Hata rais wa zamani mzee Nelson Mandela ,hakuacha kumpongeza Semenya kwa ushindi wake .Sauti yake nzito,misuli yake na kasi zake za kukimbia, zimezusha shaka shaka iwapo Semenya kweli, ni msichana. Msichana huyu wa miaka 18 na wanariadha wengine 2 walionyakua medali, walionana muda mfupi na mzee Mandela mjini Johannesberg na kupiga nae picha . Semenya alisema kuwa , ndoto yake ilikua kuonana na mzee Mandela na hakukawia kumuarifu haraka baba yake kwamba ataonana na Mandela.

Muandishi:Ramadhan Ali/ DPAE/AFPE

Uhariri: Mohammed Abdul-Rahman