1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mukwege aonya kuhusu kuondoka haraka jeshi la MONUSCO

Mitima Delachance7 Machi 2024

Aiyekuwa mgombea urais nchini Kongo Daktari Denis Mukwege, ameonya kuhusu kile anachodai ni hatari ya kujiondoa haraka kwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO, mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4dFot
Mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel Denis Mukwege
Mukwege anahofia kuwa hali mashariki ya Kongo huenda itakuwa mbaya kutokana na kujiondoa haraka MONUSCOPicha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Katika barua yake aliyoziandikia nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Daktari Denis Mukwege hakuficha wasiwasi wake kuhusu kile anachoeleza kuwa ni kuondoka kwa haraka kwa MONUSCOkatika mazingira ya vita na uvamizi wa kijeshi katika eneo hilo, hali ambayo anahisi inaweza kusababisha ombwe la ulinzi mashariki mwa Kongo.

Mukwege anahofia kuwa hali hii huenda itakuwa mbaya kwa usalama wa raia na utulivu, na hivyo kuyafanya mafanikio ya miaka ishirini na mitano ya kuwepo kwa MONUSCO kupotea bure.

Daktari huyo aliyewania na kushindwa kwenye uchaguzi wa rais wa 2023 amesema kwamba sababu kuu za vurugu bado zinaendelea kuwapo nchini Kongo, akidai kuwa ukosefu wa uhalali wa mamlaka ya Kongo, kutokujali, unyonyaji na biashara haramu ya madini, kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, utafutaji wa suluhisho za kisiasa na kidiplomasia ambayo yamesalia katika mtafaruku, kuwa miongoni mwa sababu za hali hiyo.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

Lakini chama twala cha UDPS kimeelezea kushangazwa kwake na barua hiyo ya Mukwege wakati huu ambapo ni raia wenyewe wa Kongo waliomtaka Rais Felix Tshisekedi auombe Umoja wa Mataifa uondowe askari wake nchini humo. Elie Mugisho ni miongoni mwa wasemaji wa chama cha UDPS mjini Bukavu: “Matamshi ya Bwana Denis Mukwege haishangaze wengi kati ya wakongo. Kwa sasa ni zaidi ya miaka 20 tangu uwepo wa Monusco DRC. Sijuwe ikiwa ndugu Denis Mukwege anaweza shuhudia kazi muhimu ambayo Monusco imesha fanya nchini DRC. Hawakuja tembea tu ila walikuja ili kusaidiana na jeshi la FARDC kurejesha amani lakini hadi leo hatujaishi ile amani tuliotarajia”

Na raia wa kawaida wana matazamo gani kuhusu kuondoka kwa Monusco hasa katika Jimbo la Kivu Kusini? “Tuliishi nao vizuri wakilinda raia na mali zake. Kwavile wanaondoka tufadhani kwamba polisi wataendelesha jukumu hilo la ulinzi wa raia na mali zake” Anasema Papy Matabaro. 

Naye Ladia Bunani anasema “Tunaomba polisi idhidishe pia doria kama ilivyofanya Monusco. Tatizo likitokea huku au kule wawe tayari, washirikiane na raia.”

Katika barua yake hiyo, Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2018 anaamini kwamba bado kuna wakati kwa serikali ya Kongo na Umoja wa Mataifa kusimamisha na kupitia upya mpango wa pamoja wa kujiondoa kwa MONUSCO kulingana na mabadiliko ya hali ya Kongo