1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa tatu wa shambulizi la Brussels akamatwa

Admin.WagnerD23 Machi 2016

Mmoja wa washukiwa wa mashambulizi ya jana ya mjini Brussels Najim Laachraoui amekamatwa na polisi, na ndugu wawili wakitajwa kuwa ni watuhumiwa waliojitoa muhanga katika mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/1II6B
Belgien Terroranschläge in Brüssel Fahndung Verdächtige
Picha: picture-alliance/dpa/Federal Police

Mtuhumiwa huyo aliyenaswa katika kamera akiwa pamoja na ndugu hao wawili na kabla ya kukimbia alitajwa na polisi kwa jina la Najim Laachraoui mwenye umri wa miaka 25. Wakati huo huo idadi ya vifo kutokana na mashambulizi hayo imepanda hadi 31, na wengine zaidi ya 200 wameripotiwa kujeruhiwa.

Polisi mjini Brussels, Ubelgiji wamewataja ndugu hao kuwa ni Khalid na Brahim El Bakraoui, baada ya sura zao kunaswa kenywe kamera ya uwanja wa ndege wa Zaventem kabla ya kutokea kwa miripuko miwili na baadae kutokea watatu katika kituo cha treni. Ndugu hao ni wakaazi wa mjini Brussels na wenye rekodi ya uhalifu.

Polisi wanashuku watuhumiwa hao kuwa na mahusiano na Salah Abdeslam, mtuhumiwa wa shambulizi la mjini Paris la mwezi Novemba mwaka jana.

Abdeslam alikamatwa Ijumaa iliyopita baada ya miezi minne ya msako, na alama za vidole vyake zilikutikana katika nyumba iliyokodiwa na Khalid Al Bakraoui, ambaye inaaminika alijiripua yaye na ndugu yake Brahim katika mashambulizi ya jana ya uwanja wa ndege wa Zaventem.

IS wadai kuhusika

Kundi linalojiita dola la kiislamu IS lenye makaazi yake nchini Syria limedai kuhusika na mahsambulizi hayo, siku nne baada ya kukamatwa kwa Abdeslam na polisi mjini Brussels. Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls amesema leo hii kuna haja ya kuimarisha udhibiti wa mipaka ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya baada ya mashambulizi hayo ya mjini Brussels.

"Tunakabiliwa na kitisho kikubwa cha ugaidi. Tupo katika vita. Hapa barani Ulaya kwa miezi kadhaa tumekuwa tukikabiliwa na vitendo vya kivita. Tunahitaji uhamasishaji mkubwa wakati wote dhidi ya matendo haya ya kivita," amesema Manuel Valls

Belgien Place de la Bourse Brüssel
Maombolezo mjini BrusselsPicha: Getty Images/C. Furlong

Waziri huyo aliongeza kuwa matukio hayo ya mashambulizi yanapangwa nchini Syria... ingawa magaidi hawo wanazo ngome zao nchini Ubelgiji pamoja na Ufaransa.

Mchana huu mji wa Brussels utakuwa na dakika moja ya ukimya kuomboleza waliouwawa na wote walioathirika katika mashambulizi hayo yalitokea jana asubuhi. Huku treni ya mwanzo ya kimataifa inayotokea mjini Amsterdam, Uholanzi ikiwasili mjini humo baada ya ya safari zote kusitishwa jana, mara tu baada ya miripuko hiyo kutokea.

Aidha kwa upande wa Ujerumani maafisa wa usalama wa ngazi ya juu wanasema wanataka mashirika ya usalama ya barani Ulaya yawe yakibadilishana habari za usalama kwa urahisi zaidi. Na Waziri wa mambo ya ndani wa Uherumani Thomas de Maiziere amesema mechi ya mpira ya kirafiki baina ya Ujerumani na Uingereza itakayofanyika mjini Berlin siku ya Jumamosi itachezwa kama ilivyopangwa. Na kuongeza mamlaka husika hazikugundua kitisho chochote cha usalama kinacholenga mechi hiyo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/dpae/rtre/afpe

Mhariri:Josephat Charo