1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa mkuu wa shambulizi la Barcelona atambuliwa

John Juma
21 Agosti 2017

Polisi nchini Uhispania imemtambua mshukiwa mkuu wa shambulio la Barcelona. Hayo yanajiri huku msako dhidi ya mshukiwa huyo anayeaminiwa kuwa raia wa Morocco ukitanuliwa barani Ulaya kwa jumla.

https://p.dw.com/p/2ia4g
Barcelonal Polizei Sicherheit Terror Anschlag
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Balk

Polisi nchini Uhispania imethibitisha kuwa imemtambua mshukiwa mkuu wa shambulio la Barcelona lililofanywa mwishoni mwa wiki iliyopita. Hayo yanajiri huku msako dhidi ya mshukiwa huyo anayeaminiwa kuwa ni raia wa Morocco ukitanuliwa barani Ulaya kwa jumla. Wakati huohuo idadi ya watu waliouawa kufuatia shambulizi hilo imefikia 15. Hii ni baada ya polisi kuupata mwili wa mtu aliyedungwa kisu ndani ya gari linaloaminika kutumiwa na mshukiwa kutoroka.

Waziri wa jimbo la Catalonia anayeshughulikia mambo ya ndani Joaquim Forn alisema katika mahojiano na redio ya jimbo hilo kuwa dalili zote zinaashiria kuwa mshukiwa ni Younes Abouyaaqoub, aliye na umri wa miaka 22, raia wa Morocco. Aidha polisi imetoa tahadhari na kusema huenda Abouyaaqoub amejihami na hivyo ni mtu hatari.

Picha iliyopatikana katika mtandao wa kijamii ya Younes Abouyaaquoub
Picha iliyopatikana katika mtandao wa kijamii ya Younes Abouyaaquoub Picha: picture-alliance/AP Photo/Social Media

Uchunguzi watanuliwa Ulaya

Maafisa nchini Uhispania, leo wameiarifu polisi ya Ulaya kuhusu utambulisho wa mshukiwa huyo, ili kuwezesha uchunguzi na msako dhidi yake barani Ulaya kwa jumla.

Akizungumza na wanahabari ambapo pia alionesha picha ya mshukiwa huyo mkuu, afisa mkuu wa polisi wa Catalonia Juan Ignacio Zoido alisema: "Hadi sasa juhudi za polisi zimelenga kumkamata mtu huyu, Younes Abouyaaqoub ambaye ametambuliwa kuwa dereva wa lori lilotumiwa katika shambulizi la Barcelona, na ambaye anasakwa na vyombo vya usalama vya taifa pamoja na polisi, na ninafikiri ndiyo itakuwa shughuli kuu katika siku zijazo hadi tumpate."

Inaaminika kuwa Abouyaaqoub ndiye mshukiwa pekee ambaye hajakamatwa miongoni mwa wengine 12 ambao ni wa kundi la kigaidi, na huenda yupo Uhispania au ametorokea nchi nyingine.

Gari la polisi likiondoka na mshukiwa aliyekamatwa baada ya msako mjini Ripoll
Gari la polisi likiondoka na mshukiwa aliyekamatwa baada ya msako mjini RipollPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Misako Ripoll

Forn ameongeza kuwa wachunguzi wanaolenga kundi la kigaidi, wamepiga kambi katika mji wa Ripoll, ambapo misako kadhaa imefanywa katika makaazi ya watuhumiwa, ikiwemo nyumba ya imamu mmoja kutoka Morocco Abdelbaki Es Satty ambaye anasemekana aliwapandikiza itikadi kali vijana wa Ripoll .

Imamu huyo anayeamiwa aliuwawa katika mripuko uliotokea Alcanar siku ya Jumatano wiki iliyopita, aliwahi kufungwa jela kando na kuwa wakati mmoja alikuwa pamoja na mshukiwa mkuu anayesakwa sasa kwa tuhuma za ugaidi. Polisi walipata mitungi 120 ya gesi na vifaa vya kutendeneza milipuko ndani ya nyumba yake.

Maafisa wa polisi wametangaza pia kuwa wameupata mwili wa mtu aliyedungwa kisu ndani ya gari linaloaminika kuwa lilitumiwa na mshukiwa alipokuwa akitoroka kutoka eneo la shambulizi.

Shambulio la Barcelona lilifuatiwa na jingine kama hilo eneo la Cambrils saa kadhaa baadaye ambapo polisi waliwaua washukiwa watano. Hadi sasa Jumla ya watu 15 wameuwawa na 130 kujeruhiwa katika mashambulio hayo ya Barcelona.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman