1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSaudi Arabia

Blinken, MBS wafanya 'mazungumzo ya wazi' Jeddah

Iddi Ssessanga
7 Juni 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman mjini Jeddah siku ya Jumanne, katikati mwa uhusiano ulioyumba kati ya Riyadh na Washington.

https://p.dw.com/p/4SI9I
US-Außenminister Antony Blinken in Saudi-Arabien
Picha: AMER HILABI/AFP

Saudi Arabia imekwaruzana mara kwa mara na Rais Joe Biden kuhusu ugavi wake wa mafuta ghafi kwenye soko la kimataifa, utayari wake kushirikiana na Urusi katika jumuiya ya OPEC+ na kusuluhisha mzozo wake na Iran kulikoratibiwa na China.

Biden pia aliahidi kuifanya Saudi Arabia kuwa taifa lililotengwa kuhisiana na mauaji ya mwandishi wa makala wa gazeti la Washington Post Jamal Khashoggi.

Hata hivyo Saudi Arabia kama mataifa mengine ya Kiarabu ya Ghuba, bado inaitegemea Marakani kama mdhamini wa usalama wa kanda pana ya Mashariki ya Kati, wakati mzozo kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran umesambaa na kusababisha mkururo wa mashambulizi.

Soma pia: Blinken azuru Saudi Arabia kujenga mahusiano yaliyoharibika

Riyadh na Washington pia zimekuwa zikifanya kazi pamoja kujaribu kufanikisha usitishaji wa kudumu wa mapigano nchini Sudan, ambao umeshindikana katika wiki za mapigano kati ya jeshi la taifa hilo na kikosi cha wapiganaji wenye nguvu cha RSF.

Na Saudi Arabia inataka kumaliza vita vyake nchini Yemen, jambo ambalo Marekani imelihimiza pia.

US-Außenminister Antony Blinken in Saudi-Arabien
Picha: Saudi Royal Court/REUTERS

Blinken aliwasili Saudi Arabia akiwa mwenye shauku kubwa ya kushiriki kimataifa, hasa baada ya kuhusika katika ubadilishanaji wa wafungwa katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

Washington yataraji kuimarisha zaidi uhusiano na Riyadh

Saudi Arabia ilimkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy mwezi uliopita katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, na mara baada ya hapo waziri wa mambo ya ndani wa Urusi aliewekewa vikwazo.

Wakati bei ya mafuta ikiwa chini ya dola 100 kwa pipa, utawala wa Biden hauna wasiwasi juu ya bei kwenye pampu katika msimu wa joto.

Washington huenda inatumai kuimarisha uhusiano wake wa kiusalama na Saudi Arabia kadri inavyozidi kuzijongelea China na Urusi.

Hata hivyo, Wasaudi wanaweza kutaka uhakikisho ambao Biden hawezi kutoa linapokuja suala la Bunge la Marekani kuzuwia mauzo ya silaha kwa falme hiyo.

Soma pia: Blinken ahimiza kufufua uhusiano kati ya Israel na Saudi

Blinken alikutana na Mwanamfalme Mohammed, MBS, mapema Jumatano, huku wizara ya mambo ya nje ikisema walijadili dhamira yao ya pamoja ya kuendeleza utulivu, usalama, na ustawi kote katika kanda ya Mashariki ya Kati na kwingineko.

Wizara hiyo ilisema katika taarifa kuwa waziri Blinken alisisitiza pia kwamba uhusiano kati ya mataifa hayo unaimarishwa na maendeleo juu ya haki za binadamu.

US-Außenminister Antony Blinken in Saudi-Arabien
Picha: Amer Hilabi/Pool/AP/picture alliance

Wageni wengine wa MBS

Ziara ya Blinken imekuja baada ya mshauri wa Biden kuhusu usalama wa taifa Jake Sullivan, kusafiri Jeddah mwezi Mei na kukutana na mwanamfalme Mohammed.

Mwanamfalme huyo pia  alimkaribisha Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, hasimu wa muda mrefu wa Marekani, kwa ajili ya mkutano Jumatatu jioni, kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Saudia.

Nje ya mkutano na Mwanamfalme Mohammed na maafisa wengine wa Saudi Arabia, Blinken pia atahudhuria mkutano unaolipinga kundi la Dola la Kiislamu mjini Riyadh, na kukutana na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Baraza la Ushirikiano wa Ghuba.

Kundi hilo la GCC linajumuisha mataifa sita ya Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Chanzo: Mashirika