1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wautikisa mji wa Gao

11 Februari 2013

Mripuko mkubwa umeutikisa mji wa Gao kaskazini mwa Mali saa chache baada ya mapigano baina ya jeshi la serikali na wapiganaji wa kiislamu. Awali jeshi la Ufaransa lilikuwa limetangaza kuwa utulivu umerejeshwa mjini humo.

https://p.dw.com/p/17boy
Malian soldiers stand guard on February 10, 2013 in the Malian northern city of Gao. Fights between Islamist rebels and Malian soldiers broke out in the center of Gao, recently taken over by the French military to Malian armed Islamist groups, hit by two suicides bombings within two days. AFP PHOTO / PASCAL Wanajeshi wa Mali wamekabiliana na wapiganaji wa Kiislamu ´katika mji wa Gao.
Wanajeshi wa Mali wamekabiliana na wapiganaji wa Kiislamu ´katika mji wa Gao.Picha: Getty Images

Kulingana na maelezo ya wanajeshi wa Mali, mripuko huo ulitokea kaskazini mwa mji wa Gao, kwenye kizuizi cha barabara inayoingia katika mji huo kutoka upande wa kaskazini. Kizuizi hicho kililengwa na waripuaji wa kujitoa mhanga Ijumaa na Jumamosi.

Mapambano ya bunduki kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa kiislamu katika maeneo yaliyokombolewa na vikosi vinavyoongozwa na Ufaransa jana Jumapili, ndio mapigano ya kwanza makubwa kufanywa mjini tangu kuanza kwa mgogoro huo.

Wapiganaji wa Mujao ambao wamevishambulia vikosi vya serikali
Wapiganaji wa Mujao ambao wamevishambulia vikosi vya serikaliPicha: AFP/Getty Images

Milio ya bunduki yatawala

Mirindimo ya silaha kubwa na ndogo ilitawala mji wa Gao kuanzia asubuhi hadi alasiri, na ukimya ulirejea saa za magharibi, baada ya umeme kukatwa na kuutumbukiza mji huo katika lindi la giza.

Hata baada ya hali kuwa shwari, wanajeshi wa Ufaransa na wenzao wa Mali walibakia na wasiwasi kwamba wapiganaji wa kiislamu wanaendelea kujificha mjini humo. Mkazi mmoja wa mji wa Gao alisimulia jinsi alivyoshuhudia mripuaji wa kujitoa mhanga akiuawa.

''Kulikuwa na milio ya risasi kwa takribani saa moja, kisha akajitokeza, akatembea peke yake kuwasogelea wanajeshi, akiwa na silaha. Wanajeshi walipoona anawasogelea, walimfyatulia risasi, ndio akaripuka---Boom.'' Alisema.

Vyanzo vya habari kutoka idara ya usalama vimedokeza kuwepo kwa wapiganaji wengi wa kiislamu mjini Gao, na kwamba wanajeshi wamewauwa baadhi ya wapiganaji hao. Hata hivyo, madai yao hayajathibitishwa na waandishi wa habari katika mji huo.

Bado waasi ni kitisho

Makabiliano makubwa yalianza jana asubuhi, baada ya wanajeshi wa Mali kukwaana na wapiganaji wa kiislamu katikati mwa mji, karibu na kituo cha polisi ambacho kilitumiwa na waasi kama makao yao makuu, kabla ya kutimuliwa mwezi uliopita.

Ilibidi wanajeshi wa Ufaransa waingilie kati
Ilibidi wanajeshi wa Ufaransa waingilie katiPicha: picture-alliance/AP

Shahidi mmoja alisema kuwa wanajeshi wa Ufaransa walilazimika kuingilia kati. Alisema pia kuwa kwa macho yake aliona mtu anayeamini kuwa ni raia, akipigwa risasi. Kanali wa jeshi la Mali, Mamadou Sanake, amesema kuwa waasi wamejipenyeza mjini wakitumia pikipiki, na wengine wakipita katika mto Niger ambao unapita nyuma ya ofisi ya Gavana.

Muungano wa wapiganaji wa Jihad katika Afrika ya Magharibi, MUJAO, umedai kuhusika katika mashambulizi dhidi ya wanajeshi na kuwatuma waripuaji wa kujitoa mhanga. Mashambulizi haya yanadhihirisha kitisho cha vita virefu nchini Mali huku Ufaransa ikitafakari mpango wa kufungasha virago vyake na kuondoka ikiyaacha majukumu mikononi mwa vikosi vya kiafrika. Ufaransa inataka kuondoka haraka na kuyakabidhi majukumu ya kijeshi kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda usalama, na wiki iliyopita ilitangaza kwamba itaanza kuwarudisha nyumbani wanajeshi wake mwezi Machi.

Jana, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, aliikejeli Ufaransa, akisema inavuna kile ilichopanda nchini Libya, ambako iliwapa silaha waasi waliompindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, kanali Muammar Ghadafi. Miongoni wa wapiganaji wa kiislamu kuna watuareg wengi ambao walipigana bega kwa bega na wanajeshi wa serikali ya Ghadafi, ambao baada ya kushindwa walikimbilia Mali, wakibeba silaha zao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo