1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi wa afya kwa ajili ya wakazi wa Pate

Josephat Charo
23 Oktoba 2018

Maisha visiwani yana uzuri na changamoto zake. Moja ya changamoto hizo ni kupata huduma za afya ukizingatia kuwa usafiri na ukosefu wa miundo mbinu ni vikwazo.

https://p.dw.com/p/3705p
Kenia Gesundheits NGO - Safari Doctors | Umra Omar
Umra Omar, muasisi wa mradi wa Safari Doctors, LamuPicha: DW/T. Mwadzaya

Safari ya kuelekea kisiwani Pate ilianza mapema tulipotoka Lamu mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi kabla jua kupanda na kuwa kali kadhalika bahari kukupwa. Kikosi cha madaktari kilikuwa kimeshatangulia kwa kidau chao kiitwacho Mama Daktari hadi visiwani.

Umra Omar ni muasisi wa mradi huu. Alisema, "Safari yetu huanza na Kiangwe ambako hakuna huduma za afya na inategemea wanakijiji kufunga safari kwenda kisiwani. Tukitoka hapo ndio twafika Pate Island ambapo kuna vijiji kumi na sisi huwa twapitia vijiji 5 kwa siku 2. Twaanza na pale Bahamisi, Mtangawanda ukiingia ufuo wa kisiwa. Huenda tukifika Shanga,ambako kuna Shangarubu, Shakani, tukiingia mpaka Nchundwa, Miabogi. Kwa sasa tunaangalia kama kuna namna za kupanua maana kuna jamii zinalalamika kwanini hatuwafikii. Twaingia Siyu pia." 

"Kupanda safari ya juu kwenda mpaka Mkokoni na Kiwayu kwenda mbele zaidi kuna kijiji kidogo chaitwa Madina cha wakimbizi waliokimbia vita sehemu za ndani. Yategemea usalama sasa ni safari ya gari kuuzunguka msitu wa Boni. Na hapo kijiji cha kwanza ni Mararani. Kisha Mangai tuingie Basuba tumalizie Milimani ndio tuingie Mokowe kwahiyo ni kuizunguka Lamu East nzima. Usafiri ni siku kama tatu nne tuko baharini na kisha upande wa bara inachukua kama siku mbili. Kwa hiyo tukiifunga hapa tunakwenda kabisa hakuna kwenda kurudi," aliongeza Umra. 

Kenia Gesundheits NGO - Safari Doctors
Boti la Safari Doctors likiegeshwa, Faza, kisiwani PatePicha: DW/T. Mwadzaya

Muda mfupi baada ya kusafiri kwa saa moja hivi tulikutana na maafisa wa usalama wa kikosi cha wanamaji wa Kenya waliotusimamisha na kudai vitambulisho na sababu ya safari yetu.Nahodha wetu Captain Salim anaelezea tukio hilo,” Safari imekuwa nzuri tu kwasababu tumetoka mapema maji hayana vurugu, upepo haujainuka. Kidogo nlikuwa na wasiwasi kwa sababu sikubeba kitambulisho kitambulisho nilijua watatupa shida na kutuchelwesha kwenye safari yetu. Nilitoka na haraka. Nilipigiwa simu mapema nlikuwa sijajipanga na safari nikasahau kukibeba.Kawaida kazi zetu huanzia pale Lamu na huwa sibebi kitambulisho.” 
Ifahamike kuwa jamii za Aweer na Bajuni ndio wakazi wa eneo la visiwa vya Faza, Pate, Kiwayu, Kiangwe na maeneo ya karibu yanayopakana na nchi ya Somalia upande wa baharini.Kwa sababu ya hilo maafisa wa usalama sharti wawe chonjo kuhakikisha wanaosafiri kuelekea maeneo hayo sio wahalifu. Awali safari ya kuelekea visiwani ilichukua muda mrefu kwa kutumia vidau vya kiasilia. Mambo yamebadilika. "Kawaida inachukua dakika 45 lakini pia tumekuja haraka. Hali ya hewa leo imekuwa nzuri kwasababu ilikuwa ni asubuhi na bahari haijachafuka kwahivyo ilikuwa shwari kabisa. Kila siku kazi zangu ni upande huu sasa mara kwa mara naja upande huu. Kijiji huwa tunasubiriwa kama Kiangwe huwa hawana madawa sasa sisi ni kama tumaini lao," anavyoelezea Ismail Bwana wa shirika la Safari Doctors.
Jee usafiri pamoja na madaktari hao ukoje? Clementine Logan, afisa wa mawasiliano wa shirika la Safari Doctors, anasema, "Kwavile tunalo boti letu kwa sasa liitwalo Mama Daktari, mambo yako shwari.Dawa zinahifadhiwa sehemu ya mbele ya dau. Kikosi cha wasafiri wote ni kama watu 12 ambayo si idadi ndogo. Hata hivyo sasa twaweza kusafiri kwa urahisi zaidi kutoka kisiwa kimoja hadi kingine na hilo limeimarisha huduma zetu kwa kweli."
Umra Omar ndiye muasisi wa shirika la Safari Doctors. Alielezea upeo wa safari yao ya visiwani kila mwezi."

Kenia Gesundheits NGO - Safari Doctors
Wanakijiji wa Miabogi wakisubiri huduma za afyaPicha: DW/T. Mwadzaya

Tulipowasili Faza tulielekea moja kwa moja hadi kijiji cha Miabogi walikokuwa wanasubiri wagonjwa, kina mama na watoto. Kikosi cha wahudumu 9 wa kudumu na madaktari wa kujitolea hushirikiana kila wanapotua vijijini kuwatibu wagonjwa na kugawa dawa. Fawaz Rudeiny ni daktari ambaye kwa kawaida anahudumu Mpeketoni lakini amejitolea kwenda vijijini. "Nilifurahia jinsi wao wanavyosaidia watu na wanavyotoa matibabu ya bure kulingana na kaunti ya Lamu ilivyo kijografia. Ni shida kwa watu wa hapa kupata matibabu bora mpaka wavuke bahari hadi Lamu. Pia zaidi nimefurahia mambo ya chanjo kwa watoto kwa sababu ni kitu muhimu sana. Hii ni mara yangu ya tatu, na ni ya pili mwaka huu 2018 kuandamana na Safari Doctors," alisimulia.

Ili kufanikisha safari kama hizo ipo haja ya kuwashirikisha wataalam walio na uzoefu wa muda mrefu. Harrisson Charo Kalu ndiye muuguzi mkuu kwenye mradi wa Safari Doctors. Yeye aliwahi kuhudumu eneo la Kiunga ambalo liko mbali maeneo ya baharini na upo uhaba wa vituo vya afya.

Kila wanapovitembelea vijiji na shirika la Safari Doctors alisema, "Tunakaa Lamu na tumepanga siku ambazo lazma tuwatembelee hawa ambao hawana mazahanati karibu kila mwezi. Tunawachanja watoto wadogo. Tunawahudumia kina mama wajawazito. Mikakati yetu kwa wakati huu ni mama mja mzito akipatwa na dharura tunamchukua na kumpeleka Lamu kwa dau, akishazaa na kuwa mzuri tunamrejesha kwake nyumbani. Huwa tunawaelimisha hasa kuhusu chanjo hizi za watoto ili wajue inatakikana baada ya wakati gani, inarudiwa baada ya wakati gani na zinatakikana ziwe ngapi".

Kenia Gesundheits NGO - Safari Doctors
Madaktari na wahudumu wa Safari Doctors wakiwa Miabogi, PatePicha: DW/T. Mwadzaya

Kila mwezi, kikosi hicho cha madaktari na wahudumu kinafunga safari ya kuelekea visiwani wakiwa wamejihami kwa shehena ya dawa na sindano. Kila safari wanajitahidi kuvitembelea vijiji angalau 8 na kuwafikia wagonjwa wasiopungua 800 kwa mwezi. 

Wakazi wa vijijini wamezowea kuishi karibu mno na wanyama wa nyumbani kama vile paka, punda, mbwa na kuku.Kwasababu ya hilo, viroboto huwahangaisha kila wakati kadhalika funza. Hali hii imewalazimu wahudumu wa Safari Doctors kumshirikisha daktari wa wanyama na mifugo ili kuwanusuru wakazi. Cohen Onsoti ni daktari wa wanyama na anafanya kazi pamoja na kikosi cha Safari Doctors kila wanapowatembelea wanakijiji visiwani Lamu, "Kwa wingi tunatibu mbwa, paka, mbuzi, hao ndio tunaowaona hapa zaidi. Wengi wana kupe, kunewe na kama mbwa tunawapa chanjo ya kichaa cha mbwa na pia magonjwa mengine kama mafune. Tumeona wanyama kadhaa wana kichaa cha mbwa ndio tukaanza chanjo hizo kama mwaka mmoja uliopita."

Dhamira ya shirika la Safari Doctors ni kusambaza huduma za afya mujarab kwa bei nafuu katika kaunti ya Lamu kadhalika kuyaimarisha maisha ya wakazi wa vijiji vya mbali. Je, wanakijiji wenyewe wanasemaje kuhusu huduma hizo? Mohammed Umar ni mkaazi wa Miabogi anayetatizwa na vidonda vya tumbo na punda wake pia anaumwa. "Nimekuwa nikipokea huduma hizo kwani nimetatizwa na vidonda vya tumbo kwa muda wa mwaka mmoja sasa,". Fatma, anayeishi Miabogi ana kama miezi miwili tangu aanze kutatizwa na macho na mwanawe pia alifaulu kumpeleka kiliniki kwa mara ya pili.
Muasisi wa Safari Doctors Umrah Omar na kikosi chake walivikwa taji ya maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kutoa huduma kwa wakazi wa vijiji vya mbali huko Lamu.Nilipokutana naye Umra Omra alinieleza mtazamo wake wa wanachokifanya pamoja na kuwashirikisha vijana,”Tumeona kuwa tukifanya kazi vijana kwa vijana tunakuwa na mafaniko zaidi, mazungumzo ni tofauti kidogo. Kwa sababu ni jambo lafahamika na sisi hatupo pale kusema ni sawa au si sawa. Mpira mwajua namna ya kutupata au kutaka mafunzo zaidi na tunawashirikisha mabalozi hao vijana. Sisi ni kuangalia ni mbinu gani ambazo zinaweza kuondoa hizi changamoto. Na ni watu ambao tuko kila siku. Natumai tutaweza kuwa na mabadiliko kichinichini.”
Hadi sasa kikosi cha Safari Doctors kimefanikiwa kuvitembelea vijiji visivyopungua 20 kwa vidau na safari za msituni. Shirika hilo lina mradi wa pili wa kuwashirikisha vijana kama mabalozi wa afya ili kuwahamasisha wenzao kuishi kwa uangalifu ukizingatia magonjwa ya zinaa na Ukimwi kwa jumla. Timu yao ya soka ndilo jukwaa wanalotumia kuwasogeza karibu vijana na kuwaelimisha.

Kenia Gesundheits NGO - Safari Doctors
Eneo la Faza Kisiwani PatePicha: DW/T. Mwadzaya

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Josephat Charo