Mpiga picha Anja Niedringhaus auwawa Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mpiga picha Anja Niedringhaus auwawa Afghanistan

Polisi nchini Afghanistan imesema mwandishi habari wa kike kutoka nchi za Magharibi ameuwawa kwa kupigwa risasi mkoani Khost huku mwengine akijeruhiwa vibaya siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Mpiga picha raia wa Ujerumani aliyeuwawa Afghanistan, Anja Niedringhaus Niedringhaus

Mpiga picha raia wa Ujerumani aliyeuwawa Afghanistan, Anja Niedringhaus

Msemaji wa polisi katika mkoa wa Khost,Mobarez Mohammad Zadran aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waandishi hao wawili Mpiga picha Anja Niedringhaus na muandishi Kathy Gannon walipigwa risasi leo asubuhi ndani ya makao makuu ya polisi ya wilaya na kwamba mmoja amejeruhiwa vibaya.

Zadran pamoja na naibu mkuu wa polisi wa eneo hilo Yaqub Mandozai wamesema waliofanya shambulizi hilo walikuwa wamevalia sare za polisi.

Huyu ni mwandishi habari wa pili kutoka nchi za Magharibi kuuwawa nchini Afghanistan wakati wa kampeni za uchaguzi baada ya mwandishi mwengine kutoka Sweden; Nils Horner kuuwawa kwa kupigwa risasi mjini Kabul mnamo Machi 11.

Rais wa Afghanistan anayeondoka Hamid Karzai

Rais wa Afghanistan anayeondoka Hamid Karzai

Mauaji mengine nchini Afghanistan ni ya mwandishi mkuu wa chombo cha habari cha AFP raia wa Afghanistan Sardar Ahmad, Mke wake na watoto wake wawili waliouwawa tarehe 20 mwezi Machi wakati watu waliokuwa na bunduki walipovamia hoteli ya Serena, kuwapiga risasi na kuwauwa watu tisa wakiwemo raia wanne wa kigeni.

Mkoa wa Khost unaopakana na eneo lililo na utata la Kaskazini mwa Waziristan linadhibitiwa na wapiganaji wa Haqqani wanaoshutumia kwa mashambulizi mengi makubwa nchini Afghanistan.

Mtandao wa wapiganaji hao umekuwa ukiwalenga raia wa kigeni. Kabul imetikiswa na mashambulizi makubwa wakati huu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo kesho. Uchaguzi huu ni wa kihistoria kwa kuwa ni wa kwanza utakaobadilisha madaraka kwa njia ya kidemokrasia.

Ulinzi wazidi kuimarishwa Afghanistan siku moja kabla ya uchaguzi

Aidha ulinzi umezidi kuimarishwa nchini Afghanistan kufuatia uchaguzi huo wa urais kumchagua atakayechukua kiti cha uongozi kutoka kwa rais anayeondoka Hamid Karzai, anayebanwa na katiba ya nchi hiyo kugombea tenawadhifa huo.

Kulingana na waziri wa mambo ya ndani nchini humo Omar Daudzai zaidi ya maafisa wa usalama takriban 400,000 wakiwemo polisi, majeshi, na majasusi wamewekwa kote nchini humo kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo waasi wa Taliban wameapa kuvuruga uchaguzi huo kwa ghasia na kuwahimiza wapiganaji wao kuwalenga maafisa wa uchaguzi, wapiga kura na maafisa wa usalama.

Maafisa wa Usalama Afghanistan

Maafisa wa Usalama Afghanistan

Licha ya hayo hapo jana rais Hamid Karzai amewahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa kesho.

Mchumi na mfanyakazi wa zamani wa benki ya dunia Ashraf Ghani, Abdullah Abdullah aliyejitosa katika uchaguzi wa mwaka wa 2009 pamoja na aliyekuwa waziri wa nchi za kigeni Zalmai Rassoul ni miongoni mwa wagombea 9 wanaowania kukalia kiti cha urais nchini Afghanistan.

Atakayeshinda uchaguzi na kuchukua nafasi ya Karzai atakabiliwa na kipindi kigumu cha kuiweka nchi hiyo dhabiti wakati wanajeshi wa Afghanistan wakipambana na wapiganaji wa Taliban bila ya usaidizi wa wanajeshi wa Jumuiya ya kujihami NATO. Muungano huo unaoongozwa na Marekani unatarajiwa kuondoa wanajeshi wake 53,000 nchini Afghanistan mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi:Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com