Moto waua watu 50 Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Moto waua watu 50 Ugiriki

Maafisa wanaoendeleza juhudi za kuuzima moto ambao umekuwa ukiteketeza msitu nchini ugiriki wamepata miili mingine 26. Awali watu 24 walithibitishwa kufa

Idadi ya watu ambao wamefariki dunia kutokana na moto unaoteketeza msitu mashariki mwa Athens, Ugiriki, imeongezeka na kufikia watu 50. Hii ni baada ya maafisa nchini humo kusema kuwa shirika la Msalaba Mwekundu limepata miili mingine 26 ya watu.

Afisa mmoja wa shirika la Msalaba Mwekundu ameliambia shirika la habari nchini Ugiriki, Skai, kuwa miili ya watu 26 iliyokuwa imeteketea vibaya ilipatikana katika mji wa bandari wa Rafina, idadi ambayo imethibitishwa na naibu meya wa eneo hilo, Girgos Kokkolis.

Inaonekana watu hao walifikiwa na moto walipokuwa wakijaribu kukimbilia baharini kukwepa kuungua. Haya yamejiri leo wakati maafisa wakijaribu kuwahamisha wakaazi na watalii ambao wamekwama ufukweni mwa bahari.

Waziri Mkuu Alexis Tsipras aliyelazimika kukata ziara yake ya Bosnia na Herzegovina na kurudi Ugiriki amesema watafanya kila waliwezalo kibinadamu kuudhibiti moto huo. Alexis ameendela kusema "Ni wakati mgumu kwa eneo la Attica, ni usiku mgumu kwa Ugiriki. Kwa sasa zaidi ya maafisa 600 wa zima moto wameelekezwa katika maeneo matatu makuu pamoja na magari 300."

Wazima moto, wakaazi na wanajeshi wakipambana na moto wa Rafina karibu na Athens Ugiriki

Wazima moto, wakaazi na wanajeshi wakipambana na moto wa Rafina karibu na Athens Ugiriki

Hapo awali, kituo cha redio kinachomilikiwa na serikali, ERT, kiliripoti kuwa watu 24 walikuwa wamekufa, huku kituo hicho kikinukuu duru kutoka watoa huduma za dharura za kimatibabu pamoja na hospitali.

Zaidi ya watu 150 walijeruhiwa kutokana na moto huo wa Rafina huku wengi wakiwa katika hali mbaya. Mji jirani wa Mati karibu uliangamizwa kabisa na moto huo. Kwa mujibu wa ripoti ya ERT, wavuvi, walinzi wa pwani na watalii pia wamewaokoa watu 700, kutoka ufukweni na maeneo mengine ambako walikimbilia.

Maelfu ya watu walilala ndani ya magari yao, katika kumbi za michezo au nje kutokana na hofu ya moto kuwafikia. Msemaji wa serikali, Dimitris Tzanakopoulos, amesema wanatarajia kuuzima moto huo kabisa leo.

Waziri Mkuu Tsipras ameamuru idara ya zima moto na idara nyinginezo za kutoa huduma za dharura katika majimbo jirani kutoa misaada. "Kwa sasa ni sharti sote tuwe katika hali ya tahadhari, ni lazima tuungane na tufanye juhudi kukabiliana na hali ngumu mno katika eneo la Attica na nchi kwa jumla"

Mwanamke asikitishwa na uharibifu ambao umesababisha na moto karibu na Athens

Mwanamke asikitishwa na uharibifu ambao umesababisha na moto karibu na Athens

Waziri wa Ndani, Panos Skourletis, amesema waokoaji wanaendelea kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana. Kufikia alfajiri ya leo, bado moto ulikuwa ukiteketeza msitu karibu na mji mkuu, huku moto zaidi pia ukiripotiwa kutokea katika maeneo mengine usiku wa kuamkia leo.

Hapo jana, moto pia uliripotiwa kutokea magharibi mwa mji mkuu wa Ugiriki, karibu na kivutio cha kitalii cha Kineta, wakati ambapo viwango vya joto kutokana na msimu wa jua vikiongezeka hadi nyuzi joto 40. Hali ya hatari imeshatangazwa katika maeneo ya Athens huku kukiwa na hofu kuwa huenda idadi ya vifo itaongezeka.

Tsipras amedokeza kwamba katika maeneo mengine huenda moto uliwashwa na watu walionuia kufanya hivyo kimakusudi.

Mkasa huo wa moto ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2007.

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com