MOGADISHU: Wanamgambo wazidi kukimbia ngome zao Somalia | Habari za Ulimwengu | DW | 01.01.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

MOGADISHU: Wanamgambo wazidi kukimbia ngome zao Somalia

Wanamgambo wa Kiislamu wamekimbia kutoka ngome yao ya mwisho ya Jilib karibu na mji wa Kismayu, kusini mwa Somalia.

Duru zinaarifu kwamba wanamgambo hao walikuwa wakielekea katika mpaka wa Kenya huku majeshi ya serikali yakisaidiwa na Ethiopia yakizidi kusonga mbele kuelekea Kismayu.

Wanamgambo hao wa Muungano wa Mahakama za Kiislamu walikimbia kutoka mji mkuu Mogadishu siku ya Alhamisi baada ya mapambano kati yao na wanajeshi wa Ethiopia.

Hatua ya Ethiopia kuingilia kati mzozo wa Somalia imebadilisha hali ya mambo ambapo serikali imechukua udhibiti wa maeneo kadha ambayo wiki mbili zilizopita yalikuwa yakisimamiwa na wanamgambo hao.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi amewapa wakazi wa Mogadishu siku tatu kutoa silaha walizo nazo la sivyo wapokonywe silaha hizo kwa nguvu.

Ali Gedi aliwaambia wanahabari kwamba serikali yake imepata idhini ya wananchi kutumia nguvu kuwapokonya silaha wakazi wa Mogadishu .

Mji wa Mogadishu unaaminika kuwa mji hatari zaidi na wenye silaha nyingi duniani.

Ali Gedi pia ametoa msamaha wa wapiganaji wa kiislamu wanaoelekea mpakani kati ya somalia na Kenya endapo watajisalimisha.

Hata hivyo waziri mkuu huyo amesema wakuu wa Muungano wa Mahakama za Kiislamu hawatapata msamaha.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com