1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Mapigano yarindima Somalia

23 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCh0

Mapigano inasemekana kuwa yanaendelea kurindima nchini Somalia kati ya vikosi vya Muungano wa Mahkama za Kiislam na vile vya serikali dhaifu ya mpito.

Kuna pia repoti kwamba Ethiopia imetuma vifaru na helikopta kwenye medani za mapambano kuvisaidia vikosi vya serikali.Uongozi wa Kiislam tayari unadhibiti mji mkuu wa Mogadishu na karibu sehemu kubwa iliobaki ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.Uongozi huo umetishia kutuma wanajeshi wake wa ardhini kuuteka mji wa Baidoa leo ambako ndiko yaliko makao makuu ya serikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo na kurudi kwenye mazungumzo ya amani na kujiepusha na hatua zozote zile zinazotishia suluhu na mchakato wa kisiasa.

Serikali ya mpito inadai kwamba vikosi vyake vinavyoungwa mkono na Ethiopia vimeuwa zaidi ya wapiganaji 500 wa Kiislam tokea kuzuka kwa mapigano hayo hapo Jumataano.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu madarzeni ya watu wameuwawa katika mapigano hayo na wengine wengi kuachwa bila ya makaazi.