1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moenchengladbach yatamba katika Bundesliga

2 Desemba 2013

Borussia Moenchengladbach wanaendelea na mwendo wao mzuri nyuma ya timu tatu zinazoongoza katika Bundesliga, baada ya ushindi wao wa jana Jumapili wa goli moja kwa sifuri nyumbani dhidi ya Freiburg

https://p.dw.com/p/1ARlq
Picha: picture-alliance/dpa

Raffael alifunga goli hilo la pekee na kuipa timu yake ushindi wa mechi tano mfululizo katika ligi ya nyumbani. Gladbach sasa wana pointi 28 katika nafasi ya nne, pointi nne mbele ya Schalke na tatu nyuma ya nambari tatu Borussia Dortmund. Freiburg sasa ina pointi 11 pekee na katika eneo la kushushwa daraja. Mike Hanke ni mshambuliaji wa Freiburg ambaye ni mchezaji wa zamani wa Gladach…na alipoulizwa jinsi alivyohisi kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani alisema…

"Ndiyo, nilijihisi vyema bila shaka. Nilifurahia wakati mashabiki walipoliita jina langu tena. Nilipatwa na msisimko. Lakini nimesikitika kwamba tumeshindwa leo katika uwanja huu".

Nao Hannover walirejea katika mkondo wa ushindi baada ya kuwazaba Eintracht Frankfurt mabao mawili kwa sifuri na kuwazidishia masaibu. Naye Pep Guardiola amekiri kuwa mabingwa wa Ulaya Bayern Munich walifurahia kuwazaba Eintracht Braunschweig mabao mawili kwa sifuri na kuirefusha rekodi yao ya Bundesliga kabla ya mwezi mgumu wa Desemba. Arjen Robben alitikisa wavu mara mbili na kuwapa pointi tatu, na pia kufikisha mchuano wa 39 mfululizo bila kushindwa. Kiungo wa Bayern Thomas Müller anauzungumzia ushindi wao

Mame Diouf akisheherekea bao na wenzake wa Hanover
Mame Diouf akisheherekea bao na wenzake wa HanoverPicha: Getty Images

Borussia Dortmund nao walipata ushindi wao wa kwanza baada ya mechi tatu baada ya kuwalaza Mainz 05 magoli matatu kwa moja. Roman Weidenfeller ni mlinda lango wa Dortmund. "Ni ushindi uliotokana na kazi ngumu. Hatukupenya katika mianya sawasawa. Hatukushirikiana vyema na tukaingia ndani sana bila mshikamano. Hata hivyo, ushindi unatosha. Hiyo ndio ilikuwa kazi yetu leo na tumetimiza hilo".

Nambari tatu Bayer Leverkusen waliwanyamazisha Nuremberg magoli matatu kwa sifuri wakati nao Schalke wakisonga katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi kufuatia ushindi wao wa mabao matatu wka sifuri dhidi ya VfB Stuttgart. Hata hivyo wamempoteza mchezaji wao Dennis Aogo ambaye atakuwa mkekani kwa kipindi kilichosalia cha msimu.

Werder Bremen walipata pointi moja baada ya kutoka sare ya magoli manne kwa manne na Hoffenheim katika mchuano wa kuvutia. Augsburg ambao watapambana na Bayern Jumatano wiki hii katika raundi ya tatu ya kombe la shirikisho, walitoka sare ya kutofunga na Hertha Berlin.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman