Mnangagwa aitaka UN kuangalia uchaguzi wa Afrika Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mnangagwa aitaka UN kuangalia uchaguzi wa Afrika Kusini

Mnangagwa amewataka waangalizi wa kimataifa, wakiwemo wa UN kuwa waangalizi wa uchaguzi wa taifa hilo baadaye mwaka huu.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametaka waangalizi wa kimataifa, wakiwemo wa Umoja wa Mataifa kuwa waangalizi wakati wa uchaguzi wa taifa hilo utakaofanyika baadae mwaka huu. Rais Mnangagwa ametoa matamshi hayo alipofanya mahojiano na gazeti la Financial Times la nchini Uingereza.

Mnangagwa safari hii ametumia mtazamo wa kidiplomasia zaidi tangu alipochukua madaraka mwezi Novemba mwaka jana, baada ya kuondolewa rais Robert Mugabe.

Baada ya kutangaza mapema wiki hii kwamba chaguzi zitafanyika katika kipindi cha  miezi minne hadi mitano, rais huyo mpya amewaalika waangalizi wa kimataifa kushuhudia uchaguzi huo wa Zimbabwe.

"Tunataka uchaguzi huru, wa wazi na wa haki" aliliambia gazeti hilo la Uingereza la Financial Times katika mahojiano jana Alhamisi. Aliongeza kusema "Ningependa Umoja wa Mataifa kuja kushuhudia, Umoja wa Ulaya pia wanatakiwa kuja", na iwapo jumuiya ya Madola ingeomba kuja, pia nipo tayari kuzingatia ombi lao", aliongeza Mnangagwa.

Katika miaka 37 ambayo Mugabe alitawala, waangalizi wa kimataifa walitengwa

Katika miaka 37 ambayo Mugabe alitawala, waangalizi wa kimataifa walitengwa

Waangalizi wa kimataifa hawakuruhusiwa katika chaguzi za Zimbabwe

Zimbabwe iliwatenga waangalizi wa kimataifa katika kipindi cha miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe, na katika kipindi hicho chaguzi ziligubikwa na udanganyifu wa kura na ukandamizwaji mkubwa wa upinzani.

Mnangagwa ambaye alikuwa miongoni mwa washirika wa karibu zaidi wa Robert Mugabe ndani ya chama cha ZANU-PF, amekuwa akituhumiwa kuwa na nafasi muhimu kwenye utawala wa ukandamizaji katika enzi ya Mugabe.

Lakini tangu alipochukua madaraka ya urais ameendelea kujisogeza kwa jumuiya za kimataifa, hadi kwa mtawala wake wa zamani ya ukoloni, Uingereza. Uingereza alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa uongozi wa Mugabe, ingawa Mnangagwa alitabiri kuimarika kwa mahusiano baada ya Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya mwaka ujao.

Alisema, "watatuhitaji. Na tutahakikisha tunakuwa washirika wao wa karibu sana", aliliambia gazeti hilo la Financial Times. Rais Mnangagwa pia alisema yuko tayari kuomba kurejea kwenye Jumuiya ya Madola, inayojumuisha mataifa yaliyowahi kutawaliwa na Waingereza.

ZANU-PF kimewafukuza wabunge 11

Katika hatua nyingine, chama tawala cha nchi hiyo cha ZANU-PF kimewafukuza wabunge 11 waliokuwa washirika wa karibu wa Robert Mugabe, wakati ambapo rais Mnangagwa anaendelea kuchukua hatua dhidi ya maafisa waliowaunga mkono hadharani, Robert Mugabe na mkewe Grace.

Baadhi ya wabunge waliosimamishwa kazi walikuwa mawaziri katika serikali ya zamani ya Mugabe

Baadhi ya wabunge waliosimamishwa kazi walikuwa mawaziri katika serikali ya zamani ya Mugabe

Kulingana na taarifa iliyotolewa na bunge, kuhusiana na mchakato huo ulioanza jana Alhamisi, makamu spika wa bunge Mabel Chinomona alisema ZANU-PF imeliarifu bunge kwamba wabunge hao 11 kwa sasa hawawakilishi maslahi ya chama hicho, hatua iliyochochea kufukuzwa kwao.

Baadhi ya wabunge walikuwa katika baraza la mawaziri la iliyokuwa serikali ya Mugabe. Mwezi Novemba mwaka jana, chama hicho cha ZANU-PF kilitangaza kufuta uwakilishi wa wabunge watano waliokuwa washirika wa karibu zaidi wa Mugabe, akiwemo Jonathan Moyo, ambaye alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliokuwa kwenye kundi lililokuwa likimuunga mkono Grace Mugabe.

Washirika wengi wa kisiasa wa Mugabe ama walikamatwa katika mfululizo wa matukio ya uvamizi yaliyofanywa na jeshi Novemba 15 mwaka jana, ama walikimbilia nchi jirani.

Hata hivyo, washirika wa Mnangagwa wana hofu kwamba baadhi ya wafuasi wa Mugabe wanaweza kuungana tena na kufanya kampeni dhidi ya rais huyo mpya, katika uchaguzi ujao. Moyo aliliambia shirika la habari la reuters wiki iliyopita kwamba jamii ya kimataifa inatakiwa kusaidia kuiondoa ile aliyoiita "serikali ya kijeshi" iliyongia madarakani ama kuiacha nchi hiyo iingie kwenye machafuko.

Mwandishi: Lilian Mtono, rtr.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com