1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi: Mvutano waibuka vijana CNL na Cndd FDD

Angela Mdungu
19 Agosti 2019

Mtu mmoja ameuwawa na wengine sita wamejeruhiwa katika makabiliano kati ya vijana wa chama CNDD-FDD kinachotawala nchini Burundi na wale wa chama cha upinzani cha CNL.

https://p.dw.com/p/3O8kl
Burundi Proteste in Bujumbura
Picha: AFP/Getty Images/S. Maina

Mtafaruku huo umeibuka baada ya  takribani vijana 300 wa chama cha upinzani CNL kukabiliana na  wafuasi wa chama tawala waliokuwa wamebeba mapanga wakati wakitokea katika uzinduzi wa makao makuu ya chama hicho katika mkoa wa Muyinga.

Katibu mkuu wa chama tawala, Evariste Ndayishimiye, amewataka wakuu wa tawi hilo la vijana kwenye ngazi tofauti kukaa meza moja na wenzao wa chama CNL na kujadiliana, ili kuepusha hali kama hiyo isitokee tena.

Taarifa kutoka katika kijiji cha Rugari mkoani wa Muyinga kaskazini mwa Burundi zinasema vijana wapatao 300 wa chama cha upinzani CNL waliokuwa katika uzinduzi wa makao makuu ya chama chao, walingia katika mtego wa baadhi ya vijana wa Imbonerakure wafuasi wa chama tawala waliokuwa wamebeba mapanga.

Makabiliano kati yao yalisababisha kijana mmoja wa CNL kuuawa huku wengine 6 wakijeruhiwa vibaya. Picha zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha majeruhi wenye majeraha makubwa baada ya kupigwa mapanga vichwani.
 

Nyumba zaharibiwa katika tukio jingine kama hilo

Tukio kama hilo limeripotiwa pia ambapo mapema alfajiri katika kata ya Ruziba Kusini mwa Bujumbura, vijana wafuasi wa vyama hivyo viwili wamekabiliana.

Taarifa zinasema nyumba kadhaa za eneo hilo zimebomolewa huku nyingine zikitiwa moto, ikiwemo makao ya chama hicho yaliyotarajiwa kuzinduliwa rasmi leo. Mkuu wa tarafa ya Muha, Bwana Kabura Daniel, amewatwika lawama wafuasi wa chama cha upinzani CLN ya kwamba walikiuka sheria:

Kabura amesema waliafikiana katika mikutano yao kuwa pindi chama kinapokusudia kuandaa mkutano ama shughuli yoyote ile ya kisiasa ni lazima kitaarifu mamlaka husika ili hatua za usalama zichukuliwe kuepusha vurugu, lakini chama cha CNL hakijafanya hivyo.

Mkuu wa  chama hicho, Agathon Rwasa, amekuwa akilalamika na kusema matukio kama hayo yamekithiri. Hali hiyo inajiri wakati Burundi Inajiandaa kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani, ambapo Rais Pierre Nkurunziza aliahidi kuwa hatogombea tena.

Mwandishi: Amida Issa/DW BUJUMBURA