Mlipuko wa Ebola waathiri baadhi ya michezo | Michezo | DW | 15.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mlipuko wa Ebola waathiri baadhi ya michezo

Mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola unaendelea kulitikisa siyo tu eneo la Afrika Magharibi ambalo ndilo lililoathirika zaidi bali pia ulimwengu mzima huku hofu ya kusambaa virusi ikiendelea kuongezeka.

Ni kwa hatua hiyo ambapo nchi mbalimbali zinachukua kila aina ya hatua kuhakikisha kuwa raia wake hawaambukizwi virusi hivyo na ndio maana sasa wanariadha kutoka nchi za Afrika Magharibi ambazo zimetetemeshwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wamezuiwa kudhiriki katika baadhi ya michezo ya Olimpiki kwa Vijana ambayo imeanza leo nchini China.

Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki pamoja na waandalizi wa michezo hiyo nchini China wamesema wanariadha kutoka maeneo yaliyoathirika hawatashiriki katika michezo ya kumenyana au kupigana pamoja na mabwawa ya kuogelea. Hatua hiyo ambayo inawaathiri washiriki wawili katika michezo ya kumenyana na mmoja wa kuogelea, imechukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wanariadha wengine wanaoshiriki.

Kando na hayo, wachezaji wote kutoka Afrika Magharibi watapimwa kwanza viwango vya joto mwilini pamoja na kufanyiwa vipimo vingine vya mwili wakati wa michezo hiyo. Michezo ya Olimpiki kwa Vijana inaandaliwa Nanjing, mji mkuu wa zamani wa China, kuanzia leo hadi Agosti 28, na inawashirikisha zaidi ya wanariadha 3,700 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 18.

CAF yahamisha mechi kadhaa

Na siyo michezo ya riadha tu iliyoathirika, bali pia katika kandanda ambapo sasa Mechi za kufuzu katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kuchezwa katika nchi zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola, Guinea na Sierra Leone zitahamishiwa nchi nyingine. Shirikisho la Kandanda barani Afrika CAF limesema mchuano kati ya Guinea na Togo mnamo Septemba 5 na Sierra Leone na Kongo mnamo Septemba 10 itachezwa katika nchi ambazo zitatangazwa hapo baadaye. CAF itatathmini upya hali hiyo katikati ya mwezi Septemba, huku Guinea pia ikitarajiwa kualika Ghana na Uganda mnamo mwezi Oktoba na Novemba. Sierra Leone imeomba kucheza mechi zake tatu za nyumbani - dhidi ya Kongo, Cameroon na Cote d'Ivoire - nchini Ghana.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Yusuf Saumu