Mkuu wa usalama Sudan ataka walokamatwa waachiliwe
30 Januari 2019Mkuu wa usalama wa taifa nchini Sudan ameamuru kuachiliwa huru kwa wafungwa wote waliokamatwa katika maandamano ya kupinga serikali ambayo yameitikisa nchi hiyo kwa wiki kadhaa, hata wakati ambapo waandamanaji wanapanga kufanya maandamano zaidi.
Amri hiyo iliyotolewa na Salah Ghosh imekuja huku kukiwa na ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa kwa kitengo hicho kufanya ukandamizaji mkubwa kuzuwia kusambaa kwa maandamano ambayo yalizuka kwanza mwezi Desemba.
Chama cha wataalamu nchini Sudan ambacho kinaongoza kampeni ya maandamano kimepuuzia amri hiyo ya kuachiliwa huru watu hao. Makundi ya haki za binadamu yanasema kitengo cha usalama wa taifa NISS kimewakamata watu 1,000, ikiwa ni pamoja na waandamanaji, viongozi wa upinzani, wanaharakati na waandishi habari, kama sehemu ya ukandamizaji wa maandamano hayo.