1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko ya magenge yenye silaha yaongezeka Haiti

Saumu Mwasimba
18 Mei 2022

Maelfu ya wakaazi wa mji mkuu Porta-au-Prince wameyakimbia makaazi yao kufuatia machafuko ya makundi yanayohasimiana

https://p.dw.com/p/4BSY7
Kriminalität in Haiti
Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amezungumzia hali mbaya ya usalama katika mji mkuu wa Haiti, Port-au Prince. Ameeleza wasiwasi mkubwa alionao kuhusu ongezeko la vurugu za magenge yenye silaha katika mji mkuu huo.

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Michele Bachelet amezitolea mwito mamlaka nchini Haiti kusimamia utawala wa sheria na kuwalinda wananchi kufuatia machafuko yanayosababishwa na magenge yenye silaha katika mji mkuu wa taifa hilo.

Amesema machafuko ya makundi yenye silaha nzito yamefikia viwango visivyoelezeka na hayakubaliki nchini Haiti na kwahivyo ni muhimu sana hatua za dharura zichukuliwe kurudisha utawala wa sheria na kuwalinda wananchi dhidi ya vurugu hizo pamoja na kuwabebesha dhamana wafadhili wa kiasia na kiuchumi wa magenge hayo.

Kriminalität in Haiti
Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa umeeleza kwenye taarifa yake kwamba kiasi watu 92 wasiofungamanishwa na magenge wameuliwa wakati kiasi ya watu 96 wanaodaiwa kuwa wanachama wa magenge hayo nao pia wameuliwa  wakati wa mashambulizi ya kuratibiwa na makundi yenye silaha  katika mji mkuu Port-au Prince kati ya Aprili 23 na Mei 16.

Watu wengine 113 walijeruhiwa na wengine 12 inatajwa hawajulikani waliko wakati 49 wakiwa wametekwa nyara na makundi hayo yakidai kigombozi kabla ya kuwaachilia huru. Na inaelezwa kwamba idadi halisi ya waliouwawa inawezekana ikawa kubwa kuliko hiyo iliyotolewa.

Machafuko mabaya yaliyovuka mipaka yameripotiwa katika nchi hiyo ikiwemo matukio ya watu kukatwa shingo,viungo vya mwili kukatwa katwa na maiti kuchomwa moto halikadhalika mauaji ya watoto wanaotuhumiwa kutumika kama watoa taarifa kwa magenge  hasimu. Bachelet amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu athari kubwa katika haki za binadamu zinazoikabili jamii kufuatia ongezeko hilo la machafuko ya makundi hayo yenye silaha.

UN I Michelle Bachelet
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Amebaini kwamba ongezeko la machafuko hayo limewalazimisha maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao katika kipindi cha wiki tatu zilizopita na kuzitolea mwito mamlaka za taifa hilo kuchukua hatua kwa kusaidiana na jumuiya ya kimataifa.

Kufikia sasa imeelezwa kwamba shughuli za usafiri katika eneo la  barabara mbili kuu kwenye nchi hiyo zinazounganisha mji mkuu na maeneo mengine ya nchi zimevurugwa kwa kiasi kikubwa ambapo mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Bachelet amesema hali hiyo inaweza kusababisha athari mbaya za muda mrefu katika uchumi wa taifa hilo ambao toka hapo unakabiliwa na hali ngumu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo