Mkutano wajadili Uharamia
18 Aprili 2011Huu ni mkutano wa kwanza wa daraja ya juu kupata kufanywa kati ya serikali na makampuni binafsi katika kanda ya Ghuba, kujadili njia za kukomesha vitisho vya uharamia vinavyozidi kuenea. Mkutano huo wa siku mbili, ulioitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ufalme wa Kiarabu na DP World-shirika la kimataifa linaloongoza shughuli za bandari, utajadili jithada za serikali na pia makampuni binafsi ya wamiliki meli, kukabiliana na madhara ya vitendo vya uharamia kwa mateka, familia zao, jamii kwa jumla. Vile vile vipi vitendo hivyo vya uharamia vinavyohatarisha amani na usalama kote duniani. Lengo, ni kuanzisha mpango wa ushirikiano kati ya pande zote mbili ili kuendeleza jamii,usalama na njia za kupeana habari.
Majopo maalum yatashughulikia kiini cha tatizo hilo la uharamia, masuala yanayohusika na sheria za kimataifa na uwezo wa kuendeleza ushirikiano wa kiraia na kijeshi ili kuzuia mashambulio ya maharamia. Pembezoni mwa mkutano huo, Umoja wa Falme za Kiarabu na Umoja wa Mataifa zitakuwa na kikao maalum cha kuchanga fedha kwa ajili ya mfuko maalum UN Trust Fund ulioanzishwa na Umoja wa Mataifa Januari mwaka 2010 kusaidia shughuli za kupiga vita uharamia katika mwambao wa Somalia.
Hasara kubwa kwa maisha na uchumi
Kwa mujibu wa Kituo cha Kimataifa cha Usafiri wa Baharini, tangu Aprili 14 mwaka huu 2011, kumetokea vituko 107 vya uharamia dhidi ya meli za shehena katika Ghuba ya Aden, Bahari ya Urabuni na nje ya mwambao wa Afrika Mashariki. Meli 17 zimetekwa nyara. Inatathminiwa kuwa hivi sasa maharamia wamezuia takriban meli 26 pamoja na wafanyakazi wake 532 wanaoishi katika hali mbaya. Mbali na hasara ya maisha ya binadamu, vitendo vya uharamia vinasababisha pia hasara kubwa katika biashara ya kimataifa ikitathiminiwa kufikia hadi dola bilioni 12 kwa mwaka.
Mkutano huo unaofanyika Dubai unahudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa takriban nchi zote za Ghuba na zile nchi zinazoathirika moja kwa moja kutokana na vitendo vya uharamia, kama vile Somalia, Djibouti,Comoro na Tanzania. Hata Naibu-Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mawaziri wa nje wa Indonesia, Nigeria na Pakistan wanahudhuria mkutano huo.
Mwandishi: Aryam Abraha/DW Amh/Prema Martin
Mhariri:Abdul-Rahman