1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kanada yamfunga maisha alieuwa familia ya Kiislamu

Iddi Ssessanga
22 Februari 2024

Mtu mweupe mwenye msimamo mkali alifanya ugaidi alipoigonga familia moja ya Kiislamu iliyokuwa kwenye matembezi ya jioni, hakimu wa Kanada alisema Alhamisi katika hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/4cm2R
Kanada | Mahakama Kuu
Jaji wa mahakama Kanda amemfunga maisha mzalendo wa kizungungu kwa mauaji ya kigaidi dhidi ya familia ya Kiislamu.Picha: Adrian Wyld/empics/picture alliance

 Jaji nchini Kanada alisema Alhamisi kwamba raia mzungu mwenye itikadi za kizalendi ambaye aliwagonga kwa makusudi na kuwaua watu wanne wa familia ya Kiislamu mnamo 2021 alikuwa amefanya ugaidi, uamuzi wa kwanza wa aina hiyo, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo.

Nathaniel Veltman, 23, alitiwa hatiani mwezi Novemba kwa makosa manne ya mauaji ya kukusudia ya kiwango cha kwanza, na shtaka moja la kujaribu kuua katika mauaji ya vizazi vitatu vya familia ya Afzaal ambayo pia yalimwacha mvulana mdogo yatima.

"Nimegundua kuwa vitendo vya mkosaji vinajumuisha shughuli za kigaidi," Jaji Renee Pomerance wa Mahakama ya Juu ya Haki ya Ontario alisema katika hukumu yake.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa tukio la vurugu za wazungu nchini Kanada kuchukuliwa kuwa ni kitendo cha kigaidi.

Veltman, akiendesha lori la kubebea mizigo, aliwakanyaga kwa makusudi watu watano wa familia ya Afzaal, wenye asili ya Pakistani, katika mji wa Ontario wa London walipokuwa nje kwa matembezi ya jioni mnamo Juni 2021.

Kanada | Mazishi ya wahanga wa familia ya Afzaal
Mazishi ya waathiriwa wa familia ya Afzaal waliouwa na Veltman.Picha: Nathan Denette/AP Photo/picture alliance

Waathiriwa walikuwa Salman Afzaal, 46, mkewe Madiha Salman, 44, binti yao Yumnah mwenye umri wa miaka 15, na mama wa Afzaal, Talati mwenye umri wa miaka 74.

Soma pia: Justin Trudeau amuangusha Stephen Harper Kanada

Mtoto wa kiume wa wanandoa hao mwenye umri wa miaka tisa alipata majeraha mabaya. Muda mfupi baada ya shambulio hilo, Veltman alisema: "Nimeweza. Nimewaua watu hao."

Veltman alikana mashtaka ya mauaji. Utetezi wake, ukitoa kile ulichokiita changamoto za kiakili za Veltman, ulisema matendo yake yalikuwa sawa na shtaka dogo la kuua bila kukusudia.  Mawakili wake pia walisema alikuwa katika "hali ya kuchanganyikiwa sana" baada ya kula uyoga wa kulewesha wikendi hiyo.

Jaji: Ni shambulio la kigaidi

Jaji Pomerance katika hukumu yake alisema Veltman "alikuwa amepanga shambulio la mauaji kwa miezi kadhaa na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba ataua Waislamu wengi kwa njia hii ya kikatili kadri awezavyo."

Akikumbuka kauli za Veltman kwa polisi, alisema: "Alitaka kuwatisha jamii ya Waislamu. Alitaka kufuata nyayo za wauaji wengine wa halaiki, na alitaka kuwatia moyo wengine kufanya vitendo vya mauaji." "Ninaona kwamba vitendo vya mkosaji vinajumuisha shughuli za kigaidi," alihitimisha.

Kanada Maombolezo ya familia ya Afzaal
Mwanamume akiwa ameshikilia bango baada ya mazishi ya familia ya Afzaal Juni 12, 2021.Picha: Carlos Osorio/REUTERS

Jopo la wazee wa mahakama katika kesi hiyo iliyodumu kwa takriban wiki 10 walisikia kwamba Veltman alikuwa ameandika ilani ya kigaidi," iliyopatikana kwenye kompyuta yake, ambayo ilitukuza utaifa wa wazungu na kuelezea chuki yake kwa Waislamu.

Jaji alibainisha kuwa alivalia "mavazi ya mapambano" ikiwa ni pamoja na kofia na kizibao cha kuzuia risasi wakati wa shambulio hilo.

Veltman aliipita familia ya Afzaal kwenye barabara ya London siku hiyo ya Jumapili jioni yenye joto, akageuza lori lake jipya alilolinunua likiwa limezungushiwa choko nzito, akavuka ukingo na kuwagonga.

Mauaji hayo yalikuwa shambulio baya zaidi dhidi ya Waislamu nchini Kanada tangu shambulio la risasi kwenye msikiti mmoja katika Jiji la Quebec mwaka 2017 na kusababisha vifo vya watu sita. Mhusika wa shambulio hilo la risasi hakushutumiwa kwa ugaidi.