1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe maalum wa UN aitaka Marekani kumaliza vita Syria

Sekione Kitojo
25 Novemba 2016

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria alisema jana (24.11.2016) rais wa Marekani Barack Obama anaweza kuendelea kufanyakazi hadi siku yake ya mwisho madarakani kumaliza vita nchini Syria.

https://p.dw.com/p/2TEHk
Syrien Staffan de Mistura
Mjumbe maalum wa UN katika Syria Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Urusi  haitaki  kubebeshwa jukumu  la  kuharibiwa  kwa  eneo  la  mashariki  la  Aleppo  na wakati  huo  huo mkuu  wa  kundi  la  kujitolea  la  "White Helmets" amesema  wakaazi  waliozingirwa mjini  Aleppo wana  siku  kumi  tu kabla  ya  kuanza  kufa  kwa njaa.

"Siwezi  kumdharau  rais wa Marekani  anayeondoka  madarakani kuwa  hana  nguvu  tena," Staffan de Mistura  mjumbe  maalum  wa Umoja  wa  mataifa  nchini  Syria   alisema  katika  mahojiano yaliyochapishwa  leo  katika  gazeti  la  Ujerumani  la  Sueddeutsche Zeitung.

Syrien Krieg - Kämpfe in Aleppo
Kijana mdogo akisimama huku akizungukwa na uharibifu mkubwa Aleppo masharikiPicha: Reuters/A. Ismail

"Rais Obama , na  waziri  wake  wa  mambo  ya  kigeni  John Kerry wana  nia  ya  kumaliza  msiba  mkubwa  wa  kibinadamu  katika karne  hii  ambao  umekuwao  katika  wakati  wa  uongozi  wao. Ni suala  litakalobaki  katika  muda  wao  wa  uongozi," amesema  de Mistura.

De Mistura  siku  ya  Jumanne  alieleza  wasi  wasi  wake  kwamba rais  wa  Syria  Bashar al-Assad  anaweza  kuanzisha  mashambulizi mpya  ya  kinyama  kuwasambaratisha  waasi  wanaolishikilia  eneo la  mashariki  mjini  Aleppo  kabla  ya  rais  mteule  wa  marekani Donald Trump  kuingia  madarakani Januari 20.

Amesema  mkutano  wake  wa  hivi  karibuni  mjini  Damascus ulionesha  serikali  ya  Syria  imetiwa  moyo  na  matamshi  ya Trump  wakati  wa  kampeni  za  uchaguzi  kuhusiana  na  kuacha kuwaunga  mkono  wapinzani  nchini  Syria. Lakini  amesema aliwakumbusha  viongozi  wa  Syria  kwamba  rais  yeyote  wa Marekani atakabiliwa  na  mbinyo  mkubwa  wa umma  iwapo  hali inafikia  katika  maafa  ya  kiutu  ambapo  watu 200.000 wanakabiliwa  na  njaa.

Syrien Angriffe auf Alleppo
Mashambulizi ya anga ya majeshi ya serikali ya Syria Aleppo masharikiPicha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Watu wanapungua kutokana  na vifo Aleppo

De mistura  amesema  anahofia  idadi  ya  watu  Aleppo  mashariki inaweza  kupungua  ifikapo  wakati  wa  Krismasi  iwapo mashambulizi  ya   mabomu  yataendelea, hali  ambayo  inaweza kuwalazimisha  maelfu  ya  wakimbizi  kukimbilia  Uturuki, na kusababisha   vita  vya  muda  mrefu  vya  chini  kwa  chini  katika maeneo  ya  vijijini  na  mashambulizi  ya  mabomu  katika  magari mijini.

Syrien Ahrar al-Scham Miliz
Wapiganaji wa upinzani nchini Syria wa Ahrar al-ShamPicha: Getty Images/AFP/B. al-Habibi

Mkuu  wa  kundi  la  kujitolea   nchini  Syria  linalojulikana  kama "White Helmets" Raed al Saleh  amesema  jana  wakaazi waliozingirwa  mjini  Aleppo wana siku  kumi  tu  kabla  ya  kukabiliwa na  kifo   kwa  njaa.

"Tatizo  tunalokumbana  nalo   White Helmets ,  ni  kwamba  vituo vyetu  mjini  Aleppo vimeshambuliwa na  sasa  tunafanyakazi  kama nilivyokuambia , na  vifaa  tulivyoweka  kama  vya msaada na  vifaa ambavyo  tumeweza  kuvipata  kutoka  katika  vifusi , na  vifaa ambavyo havikuharibiwa. Nafikiri  kundi  la  White Helmets, kwa mujibu  wa  taarifa  nilizonazo, linaweza  kuendelea kwa  mwezi mmoja kuwasaidia  watu walioko  katika  vifusi, hata  hivyo  hatutoi matibabu  ya  upasuaji  kama  madaktari wanavyofanya na  nafikiri hili  ni tatizo  katika  hospitali  hivi  sasa, kwa wale  waliojeruhiwa. Tunaweza kuhudumia  kwa  muda wa mwezi  mmoja  tu."

Syrien Weißhelme
Wafanyakazi wa kujitolea wa White Helmets mjini AleppoPicha: Getty Images/AFP/S. Al-Doumy

Pamoja  na  hayo  amesema  anaamini  kwamba  Urusi  haitaki kabisa  kubebeshwa  lawama  kwa  kuharibiwa  kwa  Aleppo mashariki. Wakati   huo  huo  raia 32 , ikiwa  ni  pamoja  na  watoto watano, wameuwawa  jana  katika  mashambulizi  ya  anga  ya  jeshi la  serikali  dhidi  ya  eneo  la  mashariki  la  mji  wa  Aleppo linalodhibitiwa  na  waasi.

Mwandishi: Sekione  Kitojo /  rtre

Mhariri: Yusra Buwayhid