Mizozo yazidi Venezuela | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mizozo yazidi Venezuela

Rais Maduro amekataa kuitikia shinikizo kutoka upinzani kutaka kura ya maoni kumwondoa madarakani. Njaa na mizozo inaendelea kuzua hofu. Serikali imepunguza idadi ya siku za kazi kuwa 2 pekee kila wiki.

Raia wakiwa barabarani Venezuela.

Raia wakiwa barabarani Venezuela.

Chama cha upinzani nchini Venezuela kimedai kimeshakusanya saini milioni moja kutoka kwa raia wanaotaka kura ya maoni kufanywa ili kumuondoa rais Nicolas Maduro madarakani. Hapo jana upinzani ulijaribu kumtimua afisini waziri wa chakula kufuatia upungufu wa chakula na mizozo inayolikumba taifa hilo.

Juhudi za upinzani kumtimua waziri wa chakula jana alhamisi ndiyo juhudi za karibuni katika mikakati yao kutaka kubadilisha serikali kutokana na mizozo ambapo familia zimekuwa zikipiga misururu kupokea vyakula vinavyotolewa kwa mgao. Rais Nicolas Maduro amekataa kuitikia shinikizo zinazotaka aondoke.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.

Amesema hakuna atakaye mwondoa waziri wake huku akisisitiza kupitisha mikakati mipya ya dharura kukabili juhudi za upinzani anazosema ni za hujuma dhidi ya serikali yake. "Nimesema hivi, kila kitu wanachofanya hakina ukweli kisiasa na mapinduzi yataendelea hapa na yataacha rais huyu kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii. tusipoteze muda wetu, tuwaache wafanye mambo yao".

Juhudi za upinzani

Taharuki ya kisiasa, mapungufu na ukosefu wa umeme kwa lazima ulioanza wiki hii ni baadhi ya mambo yanayohifiwa yatazidisha wasiwasi katika taifa hilo linalozalisha mafuta la Amerika Kusini.

Mbunge wa Venezuela kwa jina Ismael Garcia anayeongoza hoja ya kutimuliwa kwa waziri wa chakula Rodolfo Marco Torres amesema Venezuela inakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kuwahi tokea katika historia ya nchi hiyo.

Spika wa bunge Henry Ramos Allup amesema serikali haina budi kumwondoa waziri huyo baada ya thuluthi mbili ya wabunge kupitisha mswada wa kutokuwa na imani na waziri huyo.

Ukusanyaji wa saini kufanikisha kura ya maoni.

Ukusanyaji wa saini kufanikisha kura ya maoni.

Upungufu wa umeme

Rais Maduro hata ametishia kupunguzia wabunge nishati zaidi, kama mojawapo ya kuendeleza hatua yake ya utoaji nishati kwa mgao nchini kote. Ili kupunguza matumizi ya umeme serikali imepunguza idadi ya siku za kazi kwa wafanyakazi wa umma ambapo watafanya kazi kwa siku mbili pekee katika wiki. Hiyo ni kando na kuamuru shule kufungwa siku za Ijumaa. Serikali inasema mvua ya El Nino imesababisha mabwawa ya maji yanayozalisha umeme kukauka. Hata hivyo upinzani unasema uongozi mbaya ndio wa kulaumiwa.

Wizi na makabiliano yameripotiwa katika miji mbalimbali ukiwemo mji wa pili kwa ukubwa Maracaibo siku chache tu baada ya utoaji wa umeme kwa mgao kuanzishwa. Dayana Pereira ni mojawapo wa wafanyabiashara. "Majira ya saa nane alasiri waporaji walianza kuziba barabara, watu wakaanza kupiga kelele na kukimbia. Wakarusha mabomu ya kutoa machozi, Ilikuwa dhiki hapa, wakachoma lori pale. hawakuturuhusu kutoka nje hata na watoto."

Ikiwa tume ya uchaguzi itathibitisha kuwa saini ambazo zimekusanywa na upinzani ni halali, basi upinzani utakusanya saini nyingine milioni nne ili bodi ya uchaguzi kuandaa kura ya maoni.

Mwandishi: John Juma/ AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com