1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChad

Milio ya risasi yasikika mjini Ndjamena

Saleh Mwanamilongo
28 Februari 2024

Serikali ya Chad yatuhumu wafuasi wa upinzani kuhusika na shambulio katika ofisi za idara ya usalama wa ndani ya nchi hiyo. Shambulio hilo limeua watu kadhaa.

https://p.dw.com/p/4czQM
Wanajeshi watawanywa mjini kati huko Ndjamena baada ya shambulio kwenye ofisi za idara ya usalama wa taifa
Wanajeshi watawanywa mjini kati huko Ndjamena baada ya shambulio kwenye ofisi za idara ya usalama wa taifaPicha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Barabara zote zinazoelekea ofisi za usalama wa taifa zimefungwa leo Jumatano. Wanajeshi walitawanywa karibu na ofisi kuu ya chama cha upinzani cha Socialist Party Without Borders PSF. Serikali ya Chad imesema shambulio kwenye ofisi ya usalama wa ndani wa taifa lilikuja baada ya mwanachama wa chama cha upinzani cha PSF kukamatwa na kushtakiwa kwa jaribio la mauaji dhidi ya jaji mkuu wa taifa.

Hali ilikuwa tete katika mji mkuu N'Djamena baada ya kile serikali imekiita kuwa ni mashambulizi ya makusudi ya washirika wa mwanachama wa upinzani na wafuasi wa chama chake dhidi ya ofisi za serikali. Serikali imesema hali sasa imedhibitiwa kabisa na wahusika wa vurugu hizo wamekamatwa au wanatafutwa.

Shirika huru la kufuatilia mwenendo wa mawasiliano duniani la NetBlocks limedai kumeshuhudiwa hali ya kukosekana kwa huduma ya mtandao wa intaneti nchini Chad kuanzia mchana wa leo.

Chama cha upinzani cha PSF kinaongozwa na Yaya Dillo mpinzani mkubwa  wa rais wa mpito wa Chad pia binamu yake Mahamat Idriss Deby Itno. Dillo alikanusha  madai kuhusu  jaribio la shambulio dhidi ya jaji mkuu wa chad na kusema kwamba mitizamo hiyo ni njama ya kuwachafua upinzani.

Serikali yaonya dhidi ya vurugu kabla ya uchaguzi

Kiongozi wa upinzani Yaya Dillo akanusha madai ya wafuasi wake kumshambulia jaji mkuu wa taifa
Kiongozi wa upinzani Yaya Dillo akanusha madai ya wafuasi wake kumshambulia jaji mkuu wa taifa Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Shambulio hilo dhidi ya ofisi za usalama linakuja siku moja baada ya tangazo kwamba Chad itafanya uchaguzi wa rais Mei 6, ambao Deby Itno na Dillo wanakusudia kugombea. Yaya Dillo alikuwa mgombea wa kiti cha urais mnamo 2021 dhidi ya mjomba wake, Idris Deby Itno babake rais wa sasa Mahamat Deby.

Serikali ilionya kwamba yeyote anayetaka kuvuruga mchakato wa kidemokrasia unaoendelea nchini atachukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani.

Deby Itno alichukua madaraka nchini Chad akiwa na umri wa miaka 37 baada ya babake Idriss Deby Itno kuuawa alipokuwa akipigana na waasi mwaka 2021. Idriss Deby Itno alikuwa ameingia madarakani kwa mapinduzi na kutawala taifa hilo la jangwani kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.

Mahamat Deby Itno aliahidi kurudisha madaraka kwa raia na kuandaa uchaguzi ndani ya miezi 18, lakini akaongeza miaka mingine miwili ya mpito. Muda wa kipindi cha mpito uliongezwa hadi Oktoba 10 mwaka huu. Upinzani wa Chad umemtaka rais Mahamat Deby ambaye ni mwanajeshi kutogombea uchaguzi ujao.