1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za Genscher zakumbukwa

11 Septemba 2015

Aliekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Hans Dietrich Genscher alitoa mchango mkubwa katika kuiandaa mikutano iliyoziwezesha nchi mbili za kijerumani kuungana tena. Chama chake cha FDP kimemuenzi.

https://p.dw.com/p/1GVEq
Berlin Gedenkveranstaltung 25. Jahrestag Unterzeichnung Zwei-plus-Vier-Vertrag Genscher
Picha: picture-alliance/dpa/. Nietfeld

Tarehe 12 mnamo mwaka wa 1990 ni siku ambapo aliekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Hans Dietrich Genscher alitia saini mkataba juu ya nchi mbili za kijerumani kuungana tena.

Genscher aliitia saini hiyo kwa niaba ya Ujerumani Magharibi.Na aliekuwa Waziri Mkuu wa kipindi cha mpito Lothar de Maiziere alitia saini kwa niaba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani-Ujerumani Mashariki ya wakati huo.

Nchi nyingine zilizoutia saini mkataba huo yalikuwa madola yaliyoshinda vita kuu vya pili,Urusi, Marekani,Uingereza na Ufaransa. Na ndiyo sababu mkataba huo unajulikana pia kama 2+4 yaani nchi mbili za kijerumani na madola manne washindi wa vita.

Chama cha waliberali,FDP cha bwana Genscher kilimuenzi mwanadiplomasia huyo jumatano iliyopita mjini Berlin kwa mchango alioutoa kwenye mazungumzo yaliyofanikisha mchakato wa nchi mbili za Ujerumani kuungana tena. Hakuna sifa iliyokuwa ndogo kwa bwana Genscher kwenye hafla ya kumuenzi.

Kutiwa saini mkataba huo tarehe 12 mwezi Septemba mnamo mwaka wa 1990 kulikuwa na maana ya kukifunga kipindi cha miaka 45 ya kutenganishwa kwa nchi mbili za Kijerumani.

Katika miaka yote ya kuitumikia nchi yake kama waziri wa mambo ya nje,wakati wa vita baridi, baina ya nchi za magharibi na mashariki, Genscher alikuwa maarufu japo hakuutafuta umaarufu huo. Umaarufu ndiyo uliomtafuta mwanasiasa huyo ambae sasa ana umri wa miaka 88 akiwa katika kiti cha magurudumu.

Genscher aondoa sumu katika uhusiano

Jina la Hans Dietrich Genscher limefungamanishwa na matukio muhimu ya kihistoria ya barani Ulaya yaliyohusu kupunguza mvutano baina ya nchi za magharibi na mashariki. Jina lake linafungamanishwa na mkataba juu ya kuleta usalama na ushirikiano barani Ulaya uliotiwa saini mjini Helsinki mnamo mwaka wa 1975 .

Berlin Gedenkveranstaltung 25. Jahrestag Unterzeichnung Zwei-plus-Vier-Vertrag Genscher
Picha: picture-alliance/dpa/. Nietfeld

Mwenyekiti wa chama cha FDP,Christian Lindner aliezaliwa mnamo mwaka wa 1979, amemsifu Genscher kwa kujizatiti kwa muda mrefu katika harakati za kuondoa , Lindner alichokiita, sumu katika uhusiano baina ya mashariki na magharibi.

Genscher alikuwa Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani kuanzia mwaka wa 1974 hadi mwaka wa 1992. Sera juu ya Ujerumani mashariki iliyonzishwa na Genscher na wanasiasa wa wasocial demokrasia mwishoni mwa miaka ya 60 ilisababisha tuhuma miongoni mwa washirika wa nchi za magharibi. Pia wahafidhina nchini Ujerumani walikuwa na wasi wasi juu ya hatari ya Ujerumani kuelekea katika njia maalumu na kuelekea kuwa msikivu wa Urusi.

Katika muktadha huo,kufikiwa mkataba wa kuziunganisha tena nchi mbili za kijerumani ,kulikuwa kama muujiza. Mashaka yaliendelea kuwa makubwa hata baada ya kuanguka kwa kuta la Berlin mnamo mwaka wa 1990. Aliekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher alihofia kuungana tena kwa nchi mbili za kijerumani.

Licha ya tuhuma na shutuma hizo juu ya siasa ya Genscher kuhusu Ujerumani Mashriki, mwanadiplomasia huyo alifanikiwa kuyaondoa mashaka yote ya washirika wa magharibi.

Mnamo mwaka wa 1991 Urusi iliuidhinisha mkataba juu ya kuungana tena nchi mbili za kijerumani. Hilo lilikuwa taji la ushindi kwa siasa ya Genscher. Jina la Genscher pia linafungamanishwa na harakati zilizolenga shabaha ya kuziondoa silaha za nyuklia duniani.

Juu ya bara la Ulaya Genscher alitoa mwito wa mshikamano.Alisema mambo hayataweza kuwa mazuri daima kwa Wajerumani, ikiwa yanazidi kuwa mabaya kwa jirani.

Mwandishi:Fürstenau,Marcel

Mfasiri:Mtullya abdu.

Mhariri: Gakuba Daniel