1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo mkubwa kabisa waitikisa Ufaransa

Oumilkheir Hamidou
5 Desemba 2019

Shughuli za usafiri zimesita, shule zimefungwa, na katika mnara wa Eifel hakuna watu baada ya vyama vya wafanyakazi kuitisha migomo kupinga mipango ya serikali ya kuufanyia marekebisho mfumo wa pensheni

https://p.dw.com/p/3UG7t
Frankreich landesweiter Streik gegen Reformpläne
Picha: Reuters/Tessier

Jiji la Paris limetuma askari polisi 6000 kwa kile kinachotajwa kuwa maandamano makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika mji mkuu huo wa Ufaransa-mikusanyiko ya watu waliomkasirikia rais Emmanuel Macron na mpango wake wa mageuzi ya mfumo wa pensheni wanayosema utahatarisha mtindo wao wa maisha walioupigania.

Mnara wa Eifel na Kumbusho la Louvre wamewaonya watalii dhidi ya vurugu zitakazosababishwa na mgomo huo na hoteli za mjini Paris zinatapa tapa kupata wageni. Wageni wengi-ikiwa ni pamoja na waziri wa nishati wa Marekani-wamefutilia mbali mipango ya kuitembelea nchi hiyo ambayo ni mojawapo ya nchi zinazotembelewa na watu wengi zaidi ulimwenguni.

Baskeli na mguu ndio njia pekee iliyosalia ya usafiri Paris
Baskeli na mguu ndio njia pekee iliyosalia ya usafiri ParisPicha: Reuters/G. Fuentes

Safari za metro, mabasi na ndege zimesitishwa

Vituo vya safari za reli ya chini kwa chini katika jiji la Paris, vimefungwa na kuzidisha vurugu katika shughuli za usafiri ambazo tokea hapo ni za vurugu.Wafanyakazi wengi wa Paris na vitongoji vyake wanafanyakazi majumbani au wameamua kutokwenda kazini ili kusalia na watoto wao majumbani kwakuwa asili mia 78 ya waalimu wa jiji hilo wamejiunga na mgomo huo.

Vituo vya kihistoria vya treni vitupu na treni moja kati ya kumi  za mwendo wa kazi ndio inayofanyakazi. Safari nyingi za ndege katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaule zimefutwa kwakuwa shirika la ndege la Air France limefuta takriban asili mia 30 ya safari za ndani.

Wakijiandaa kukabiliana na uwezekano wa kutokea machafuko na uharibiifu katika mitaa ya mji mkuu Paris, Polisi wamewatolea wito wafanyabiashara wafunge mikahawa na vituo vyengine ya kibiashara. Maafisa wa serikali wametangaza marufuku ya watu kuandamana katika mtaa mashuhuri wa Champs Elysée, karibu na kasri la rais, bunge na karibu na kanisa kuu la Notre Dame. Wanaharakati wa vizibao vya manjano wamejiunga na vyama vya wafanyakazi kuandamana mjini Paris na katika miji mengine kote nchini humo-wakipania kushinikiza madai yao kuhusu haki sawa za kiuchumi.

Mwanaharakati wa vuguvugu la vizibao vya manjano akibeba bango lililoandikwa "Hasira"
Mwanaharakati wa vuguvugu la vizibao vya manjano akibeba bango lililoandikwa "Hasira"Picha: Getty Images/AFP/Z. Abdelkafi

Wafanyakazi wanahofia mageuzi ya mfumo wa pensheni yatafuja mtindo wao wa maisha

Watumishi wa mashirika ya umma wanahofia mageuzi ya pensheni rais Macron aliyodhamiria kuyaanzisha yanaweza kuwalazimisha wafanye kazi muda mrefu zaidi na pia kuwapunguzia malipo ya uzeeni. Wanasema haya ni mapambano ya haki ya kulinda mtindo wao wa maisha.