Merkel na Westerwelle ni timu ya aina gani? | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 10.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Merkel na Westerwelle ni timu ya aina gani?

Kansela mwenye nguvu na waziri wa mambo ya nje asiye na uzoefu, je muungano huo umekwenda vipi ndani ya miaka minne iliyopita nchini Ujerumani?

Kwa Guido Wetserwelle kuhama kutoka katika kambi ya upinzani bungeni na kukwea ngazi kufikia nafasi ya juu kabisa ya wizara ya mambo ya nje ulikuwa ushindi mkubwa.

Mwanasiasa huyo, ambaye kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa chama cha FDP aliyechekwa, alikipatia chama chake asilimia 15 ya kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009, jambo ambalo halikuwa limewahi kutokea kabla.

Westerwelle alikuwa amefika katika kilele cha mamlaka: Alipewa wadhifa wa waziri wa mambo ya nje na naibu kansela. Lakini hata kwake mwanzo ulikuwa mgumu. Westerwelle alijihusisha zaidi na siasa za ndani badala ya kushughulikia wizara yake.

Lakini mwaka 2011 aliuachia uenyekiti wa chama na cheo chake cha naibu kansela na kujikita hasa katika majukumu yake kama waziri. Kwa mtazamo wa mwenyekiti wa kamati inayoshughulikia sera za nje bungeni, Ruprecht Polenz, hatua hiyo imemsaidia Westerwelle kupata mafanikio.

"Nadhani haashirii tu, bali kila mtu anaona wazi kwamba yeye ni waziri wa mambo ya nje kwa moyo wote na kwamba anaelewa mada zinazomhusu. Anajaribu kupeleka mbele msimamo wa wajerumani katika bara la Ulaya. Yeye ni mtu mwenye imani na mahusiano baina ya nchi moja na nyingine. Hii ina maana kwamba hataki Ujerumani ifanye mambo yake pekee yake." Anasema Polenz.

Bado Westerwelle si mzoefu

Viongozi wakuu wa Ujerumani na Ufaransa kwenye mkutano wa kilele wa NATO mwaka 2012. Guido Westerwelle (kushoto) bega kwa bega na Merkel.

Viongozi wakuu wa Ujerumani na Ufaransa kwenye mkutano wa kilele wa NATO mwaka 2012. Guido Westerwelle (kushoto) bega kwa bega na Merkel.

Hata hivyo, ni dhahiri kwamba Westerwelle bado hajafikia kiwango cha uzoefu kama Kansela Angela Merkel. Kwa mtazamo wa Günther Hellmann, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa, Westerwelle hana nafasi kubwa ya kuonyesha uwezo wake pembeni mwa Merkel.

"Hivi sasa amekuwa waziri wa mambo ya nje mwenye nguvu. Hata hivyo zamani hakuwa hivyo. Ni vigumu sana kwa waziri wa mambo ya nje kuwa na Kansela ambaye ameshaizowea kazi yake na ambaye kila anapotoa tamko la serikali anafanya kwa namna ambavyo anajua itamletea mtazamo mzuri kwa watu." Anasema Hellmann.

Mtaalamu huyo anaongezea kwamba mbali na hayo, tangu kusainiwa kwa mkataba wa Lisbon, mamlaka mengi yaliyokuwa chini ya wizara ya mambo ya nje yamehamia katika ofisi ya kansela. Wachambuzi wanaeleza kuwa Merkel anaelewa namna ya kumsukumia waziri wa mambo ya nje maamuzi yanayoweza kuleta utata.

Hilo lilionekana wazi katika uamuzi wa mgogoro wa Libya Machi 2011. Westerwelle hakupiga kura kuunga mkono au kupinga kupiga marufuku ndege kuruka juu ya anga ya Libya. Kwa uamuzi huo, Westerwelle alikosolewa vikali na wapinzani wake wa kisiasa na vile vile na vyombo vya habari.

Amejifunza vya kutosha

Kiongozi wa FDP, Phillip Rösler (kushoto), aliyekuwa Rais wa Ujerumani, Christian Wulff (katikati) na Guido Westerwelle.

Kiongozi wa FDP, Phillip Rösler (kushoto), aliyekuwa Rais wa Ujerumani, Christian Wulff (katikati) na Guido Westerwelle.

Mtaalamu wa siasa za nje kutoka chama cha SPD, Rolf Mützenich, anakubaliana na ukweli kwamba Westerwelle ameongeza ubora kadri miaka yake uongozini ilivyoongezeka. Hata hivyo anaeleza kuwa kwake ni vigumu kusema ni wapi Westerwelle alipotilia mkazo katika siasa zake za nje.

"Kitu nisichoweza kukikubali kabisa na ambacho sikielewi ni kwa nini hakusema lolote juu ya uuzwaji wa silaha nje ya nchi. Nadhani hapa waziri wa mambo ya nje alipaswa kuchukua nafasi nyingine, hasa anaposema kwamba anaunga mkono siasa ya sera za nje zenye ushirikiano."

Mützenich amekosoa pia kuwa Westerwelle alishindwa kumuunga mkono rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev aliyejaribu kuweka sera mpya za usalama wa kimataifa.

Westerwelle anagombea tena nafasi ya kuingia bungeni kupitia tiketi ya chama chake cha FDP.

Mwandishi: Bettina Marx
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com