Mdahalo Kenya wawabana wagombea | Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2013 | DW | 12.02.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2013

Mdahalo Kenya wawabana wagombea

Wagombea wa kiti cha urais nchini Kenya jana (11.2.2013) walikalia kitimoto katika mdahalo wa wazi juu ya mustakabali wa nchi hiyo katika uchaguzi wa tarehe 4 Machi.

Kenia Frauen Politik 2007

Kenia Frauen Politik 2007

Hii ni mara ya mara ya kwanza katika historia ya Kenya, wagombea urais kwenye uchaguzi ujao wamepata nafasi ya kushiriki kwenye mdahalo wa pamoja na kujibu maswali kutoka kwa wananchi juu ya maono yao na mipango yao ya uongozi wa nchi punde watakapochaguliwa tarehe nne mwezi ujao.

Mdahalo huo ambao umeonyeshwa moja kwa moja kupitia vituo vyote vinane vya televisheni na zaidi ya vituo 30 vya redio nchini Kenya, umewaleta pamoja wagombea wote wanane wa kinyang'anyiro cha urais, Raila Odinga Uhuru Kenyatta, Musalia Mudavadi, Peter Keneth, James Ole Kiyiapi, Martha Karua ambaye ni mgombea wa pekee wa kike, Paul Muite na Mohammed Abduba Dida.

Kwa muda wa saa nne unusu wagombea hao wa kiti cha urais walikuwa na wakati mgumu kueleza sera zao na kujibu maswali kutoka kwao wenyewe kwa wenyewe, viongozi wa kipindi na watazamaji.

Asiyekubali kushindwa si mshindani

Jambo lililowafurahisha watazamaji ni kwamba washiriki wote wanane wanaowania wadhifa wa urais wameapa kwamba watakubali matokeo ya uchaguzi na ikiwa kuna yeyota ambaye hataridhika ataenda mahakamani.

Mgombea wa muungano wa Cord Raila Odinga alikuwa wa kwanza kukiri hayo. “Tumesema kama CORD tutakubali matokeo ya uchaguzi huu tukishindwa tutakubali kushindwa na kama tunamalamishi tutaenda mahakamani”

Raila Odinga, mgombea wa muungano wa CORD

Raila Odinga, mgombea wa muungano wa CORD

Naye mgombea wa pekee wa kike kwenye kinyang'anyiro hicho Martha Karua akitoa matamshi sawa" alisema Odinga. Kwa upande wake Karua alisema “Ni sharti tufuate sheria na kama kuna mtu ambaye hataridhishwa na matokeo aende mahakama”.

Vile vile Musalia Mudavadi, Uhuru Kenyatta, Peter Keneth na Paul Muite matamshi yakawa ya kwamba asiyekubali kushindwa si mshindani. “Tunataka kushinda lakini hatimaye tutakuwa na mshindi mmoja pekee kwa hivyo ni sharti tujiandae kukubali kushindwa endapo mwingine atashinda” alisema Kenyatta.

Kauli nyingine zilizosikika vinywani wa wagombea hao ni pamoja na "Ifikapo tarehe 4 Machi, sina shida kukubali kushindwa ikiwa itakuwa hivyo” pamoja na “Mwaka 2002 nilikubali kushindwa na Mheshimiwa Mwai Kibaki na wakati huu sina budi kufanya hivyo endapo nitashindwa”.

Kenyatta na kizungumkuti cha ICC

Kenyatta ambaye anakabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC alisisitiza kuwa mashitaka hayo hayawezi kuwa kikwazo katika uwezo wake wa kuiongoza nchi. Kesi ya Kenyatta ilikuwa ni miongoni mwa masuala yaliyozua maswali mazito mojawapo likiwa ni hatima ya Kenya ikiwa mwanasiasa huyo atapatikana na hatia.

Uhuru Kenyatta mgombea anayekabiliwa na kesi ICC

Uhuru Kenyatta mgombea anayekabiliwa na kesi ICC

Wanachi wapatao 200 wa Kenya ambao walihudhuria katika ukumbi wa mdahalo ni miongoni mwa wale waliopaza sauti kuhusu suala la ICC na ugombea wa Kenyatta.

Naye Waziri Mkuu Raila Odinga, ambaye ndiye mgombea mwenye mvuto kwa wengi kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, alisema kuwa nchi haiwezi kuongozwa na mtu aliye mbali. "Itakuwa ngumu sana kuendesha serikali kwa kutumia Skype kutoka The Hague" alisema Odinga.

Licha ya hayo, Kenyatta mwenye alisisitiza kuwa ataweza kumudu suala hilo. " Kama watu wa Kenya watanichagua kuwa rais wao, nitaweza kumudu suala la kusafisha jina langu wakati huohuo nikihakikisha kuwa uongozi wa serikali unaendelea na ajenda zetu kwa ajili ya Kenya zinatekelezwa", alisema Kenyatta.

Maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya

Maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya

Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto wanatuhumiwa kuhusika na mchafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1000 na wengine maelfu kupoteza makaazi yao. Mashitaka dhidi ya Kenyatta yanahusisha pia uhalifu dhidi ya ubinaadamu kutokana na mauwaji ya watu, mateso na vissa vya ubakaji dhidi ya wafuasi wa rais wa sasa wa nchi hiyo Mwai Kibaki.

Masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na ukabila, uongozi, ufisadi, usalama, afya na elimu yamejadiliwa kwa kina kila mgombea akitoa mikakati yake ya kukabiliana na maswala hayo. Mdahalo mwingine kama huo utaandaliwa tarehe 25 mwezi huu, wiki moja kabla kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Mwandishi: Alfred Kiti DW - Nairobi

Mhariri: Stumai George

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com