1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May azidi kuandamwa

16 Novemba 2018

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May amejaribu kuutetea muswada wa mpango wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, mchakato unaoitwa Brexit, kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa mawaziri wake waandamizi.

https://p.dw.com/p/38MDM
England | PK Theresa May
Picha: Getty Images/AFP/M. Dunham

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May amejaribu kuutetea muswada wa mpango wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, mchakato unaoitwa Brexit, kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa mawaziri waandamizi pamoja na jaribio la baadhi ya wajumbe wa chama chake cha Conservative kuanzisha mchakato wa kumuengua kama kiongozi wa chama na kumchagua kiongozi mwingine.

Mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa Brexit kutoka ndani ya chama chake Jacob Rees-Mogg, awali alipendekeza kupigwa kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu huyo wa Uingereza.

Rees-Mogg anayeongoza taasisi ya Ulaya inayojihusisha na tafiti kuhusu Brexit na inayounga mkono hatua hiyo, aliandika kwamba mpango wa May umeshindwa kukidhi ahadi alizozitoa kwa taifa hilo.   

Wabunge 48 wa chama cha Conservative watapaswa kusaini barua za kutokuwa na imani na Bi May, ili kuruhusu kupigwa kura bungeni ya kutokuwa na imani na waziri mkuu huyo. Rees-Mogg amesema kumekuwepo na ongezeko la wabunge wanaosaini barua hiyo, hasa baada ya kutangaza kuiwasilisha barua yake.

UK Brexit | Parlament - Jacob Rees-Mogg
Mbunge Rees-Mogg anayeleta changamoto kubwa na kuhamasisha kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/A. Dennis

Changamoto inayomkabili waziri mkuu May, inafuatia hatua ya baadhi ya mawaziri wa serikali yake kujiuzulu nyadhifa zao hapo jana, wakipinga muswada wa mpango wa Brezit ulioandaliwa pamoja na Umoja huo.

Miongoni mwa mawaziri hao ni, Dominic Raab, aliyekuwa waziri anayehusika na Brexit, waziri wa ajira na pensheni, Esther McVey, naibu waziri wa masuala ya Ireland Kaskazini, na naibu waziri aliyeshughulikia Brexit, Suelle Braveman.

Raab aliandika kwenye barua yake ya kujiuzulu aliyoiwasilisha kwa waziri mkuu May, akisema "kwa nia njema asingeweza kukubaliana na masharti yaliyopendekezwa kwenye mpango huo wa Brexit na Umoja wa Ulaya."

Baraza la mawaziri la May lilipitisha muswada huo siku ya Jumatano, lakini wabunge kutoka vyama vyote waliukataa wakati wa mjadala wa bunge jana

UK Brexit | Ministerpräsidentin Theresa May im Unterhaus
Wabunge wengi wanaonyesha kutomuunga mkono May na mapendekezo yake kuhusu BrexitPicha: picture-alliance/empics/PA Wire

Wabunge wa Conservative wanaounga mkono Brexit walisema haukuonyesha matokeo yaliyotarajiwa na Waingereza wengi waliopiga kura ya kuunga mkono kujiondoa kwenye Umoja huo, katika kura ya maoni ya mwaka 2016. Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbin alisema muswada huo ulikuwa haujakamilika na kuahidi chama chake kitaupigia kura ya kuupinga.

May anahitaji uungwaji mkono mkubwa bungeni ili kupitishwa muswada huo, baada ya kuridhiwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya. Lakini kuongezeka kwa upinzani kutoka kwa wabunge kunaibua wasiwasi kuhusu iwapo utapitishwa.

Makubaliano kati ya chama cha Conservative cha waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May na chama cha DUP cha Ireland Kaskazini juu ya mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, ama Brexit huenda yakafikia tamati, iwapo May ataendelea kuwa kiongozi wa chama hicho.

Gazeti la Uingereza la Telegraph Daily limeripoti likinukuu chanzo kilicho karibu na kiongozi wa chama cha DUP Arlene Foster kwamba Chama hicho kimesema, hakitapigia kura makubaliano hayo yatakapoletwa bungeni, na kuongeza kuwa uungaji wake mkono hivi sasa utategemea ni nani atakayekuwa kiongozi wa chama hicho cha Conservative.

Vingozi wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kukutana mjini Brussels, ifikapo Novemba 25, kwenye mkutano maalumu wa kilele kujadili makubaliano ya muswada huo. 

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: