1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa SADC wajadili namna ya kuimarisha uchumi

Hawa Bihoga, Dar es Salaam29 Mei 2020

Nchi kumi na sita zinazounda jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC zinajadili uwezekano wa kuondoa vikwazo mipakani kutokana na janga la virusi vya corona. 

https://p.dw.com/p/3czWG
Tansania SADC Ministertreffen Videokonferenz
Picha: Office of the Prime Minister of Tanzani

Mkutano huo wa baraza la mawaziri umetanguliwa na mwingine ulioahusisha makatibu wa kuu kutoka mataifa yanayounda jumuia hiyo ambao walijadili takriban ajenda nane ikiwemo, mwenendo wa maabukizi ya virusi vya corona ndani ya nchi wanachama, hali ya biashara, viwanda huku hoja ya uchukuzi ikichukua mjadala mpana zaidi hata katika baraza hili la mawaziri.

Wakitathmini mafanikio ya itifaki na muongozo wa usafirishwaji wa huduma na bidhaa ulioowekwa kwa takriban siku hamsini sasa tangu kuzuka kwa maambukizi ya corona ndani ya jumuia, imebainika kuwepo na changamoto kadhaa hususan katika mipaka, hatua ilioamuliwa kuundwa kwa kamati itakayoshughulikia changamoto hizo na hatimae huduma kuendelea katika hali ya kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa baraza hilo ambae pia ni waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki nchini Tanzania Profesa Paramagamba Kabudi amesema, kumejitokeza changamoto katika utekelezwaji wa kanuni za pamoja katika suala la usafirishaji wa huduma na bidhaa muhimu jambo ambalo litashughulikiwa kwa haraka ili kurejesha hali ya kawaida katika huduma ya usafirishaji. 

Lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kuondoa vizuizi vya mpakani kutokana na janga la corona ili kuwezesha usafiri na uchukuzi baina ya mataifa kwenye jumuiya hiyo.
Lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kuondoa vizuizi vya mpakani kutokana na janga la corona ili kuwezesha usafiri na uchukuzi baina ya mataifa kwenye jumuiya hiyo.Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Changamoto ilioonekana kuhitaji ufafanuzi wa haraka ni kati ya Tanzania na Zambia ambapo hivi karibuni, serikali ya Rais Edgar Lungu iliamua kuuweka mji wa Nakonde katika karantini ilikuzuia kasi za maambukizi ya virusi vza corona hatua iliotafsiriwa na wachambuzi wa diplomasia kuwa ukiukaji wa itifaki ya usafirishaji katika jumuia.

Waziri wa uchukuzi nchini Tanzania muhandisi Isaack Kamwelwe ameiambia DW kuwa Zambia ni miongoni mwa washiriki katika mkutano huo ambapo, baraza hilo la mawaziri litalitolea ufumbuzi swala hilo lililodhoofisha itifaki ya usafirishaji kadhalika kuathiri idadi kubwa ya watu wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo la mpakani.

Aidha baraza hilo la mawaziri limeridhia kwa pamoja kuwa na orodha ya idadi ya makampuni katika nchi wananchama zanazofanya uzalishaji wa bidhaa za kujikinga na virusi vya Corona kama vile, vieuzi, barakoa pamoja na mavazi ya wahudumu na kusambaza kwa nchi wananchama ambapo kila taifa litatakiwa kununua vifaa kutoka katika kampuni hizo.