1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauwaji ya Kasai na madai ya kuachana na CFA magazetini

Oumilkheir Hamidou
31 Machi 2017

Kisa cha kuuliwa watumishi wawili wa Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,hatima ya faranga CFA na desturi za watu kubugia udongo wa kinamo ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2aPr3
Kongo Kananga Tshimbulu MONUSCO
Picha: Reuters/A. Ross

 

Tunaanzia maziwa makuu , katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ambako malumbano na mapambano yamepamba moto dhidi ya serikali. Kwa kuwauwa watumishi wawili wa Umoja wa mataifa na wanajeshi, kundi moja la waasi wa kabila dogo la Bajila Kasanga linataka kueneza vitisho  na kutangaza vita dhidi ya serikali ya rais Joseph Kabila mjini Kinshasa, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Wataalam hao wawili wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wametumwa na katibu mkuu Antonio Guterres, Michael Sharp wa Marekani na  Zaida Catalan, rais wa Sweden mwenye asili ya Chili walitekwa nyara katika mkoa wa Kasai, kati kati ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, eneo linalogubikwa na mashambulio ya kundi la waasi la Kamwina Nsapu. Frankfurter Allgemeine linakumbusha katika eneo hilo hilo ndiko walikotekwa nyara mwishoni mwa wiki iliyopita na baadae kuuliwa kwa kukatwa kichwa askari polisi 39. Baada ya kuutaja utajiri wa  almasi wa mkoa wa Kasai, Frankfurter Allgemeine linajiuliza sababu gani hasa inapelekea kutokea ukatili ambao hauna mfano katika maeneo mengine ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo? Sababu halisi inakutikana katika kinyang'anyiro cha kuania madaraka ndani ya kundi hilo la waasi la Kamwina Nstapu baada ya kiongozi wake  wa zamani kufariki.

Baraza la Usalama lapanga kupunguza wanajeshi 500 wa kikosi cha kulinda amani Kongo Kinshasa

Wataalam 2 wa Umoja wa Mataifa wameangukia mhanga wa mapambano ya kuania madaraka linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine linalokumbusha tume ya Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imekuwa ikiendesha shughuli zake tangu miaka 17 iliyopita-wakihusishwa wanajeshi na raia 19 000 na kuigharimu jumuia ya kimataifa dala bilioni moja kwa mwaka. Frankfurter Allgemeine linamaliza kwa kuzungumzia mpango wa baraza la usalama la umoja wa mataifa wa kupunguza wanajeshi 500 toka kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa katika jamahuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Nchi za kiafrika zinazozungumza kifaransa kuachana na sarafu ya faranga CFA

"Ni suala la Mamlaka yetu" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Neues Deutschland linalozungumzia juhudi za nchi za kiafrika za kutaka kujitoa katika mfumo wa sarafu ya Faranga. Faranga CFA imeanzishwa mwaka 1945 katika nchi za kiafrika zinazozungumza kifaransa hata kabla ya nchi hizo kupata uhuru . Hivi sasa sarafu hiyo ya Faranga CFA inaunganishwa na sarafu ya Euro na kudhaminiwa na Ufaransa. Mataifa ya Afrika yanayozungumza kifaransa yanapigania kuachana na faranga CFA. Neues Deutschland linajiuliza kwanini nchi hizo 14 za Afrika zinazojivunia sarafu yenye nguvu, zinataka kuwa na sarafu nyengine? Jibu la suala hilo, lina ncha nyingi: Ndogo Samba Sylla, mtaalam wa masuala ya kiuchumi aliyehojiwa na gazeti la Neues Deutschland anajibu kwa kuzungumzia kwanza sababu za kiuchumi-sarafu ya CFA haina nguvu kwasababu inaunganishwa na Euro.

Ukuaji wa kiuchumi katika kanda ya Euro hauzifaidishi hata kidogo nchi zinazotumia sarafu ya CFA. Uchumi wa mataifa ya Afrika una yumba yumba kwasababu unategemea zaidi bei za mali ghafi na shughuli za kilimo zinazotegemea pia hali ya hewa namna ilivyo. Suala kama mataifa mengi yanaunga mkono kubadilishwa sarafu ya faranga CFA amelijibu kwa ndio na kusema majadiliano yamepamba moto katika miji mikuu kadhaa ya Afrika na hata nchini Ufaransa kwenyewe. Neues Deutschland limemnukuu mtaalam huyo wa masuala ya kiuchumi akimtaja rais wa Chad, Idriss Deby aliyelizusha suala hilo la kubadilisha mfumo wa sarafu tangu mwaka 2015. Rais Macky Sali wa Senegal ambae awali alikuwa akiitaja sarafu ya faraanga CFA kuwa ni sarafu ya maana, ameweza kubadilisha msimamo wake baada ya kutanabahishwa na wataalam wa kiuchumi. Hoja nyengine inayotolewa dhidi ya sarafu ya faranga CFA ni kwamba nchi za Afrika ziachiwe zidhamini wenyewe mustakbali wao" linamaliza kuandika Neues Deutschland.

 Udongo wa Kinamo na faida zake

Ni gazeti hilo hilo la Neues Deutschland linalotukamilishia ukurasa wetu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani kwa ripoti kuhusu desuri za watu kupenda kubugia aina fulani ya udongo unaojulikana kama ugondo wa kinamo. Desturi hizo zimeenea barani Afrika na hasa miongoni mwa wanawake wajawazito na wanawake wengine. Neues Deutschland linasema hata kama hakuna utafiti uliofanywa, hata hivyo huenda udongo huo una maadini ya kinga kwa mwili wa binaadam.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman