1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya vijana Mombasa yazusha mjadala

Eric Ponda20 Septemba 2018

Vijana wasiopungua sita wameuawa na polisi ndani ya muda wa wiki mbili zilizopita na kisa cha hivi punde kabisa kikiwa kile cha kuuawa kwa kijana aliyepigwa risasi Jumatano asubuhi.

https://p.dw.com/p/35EYy
Mombasa Anschlag auf radikal islamischen Prediger Ibrahim Ismail
Picha: Getty Images/AFP

Kwa mara ya kwanza kabisa kumezuka tofauti miongoni mwa mashirika ya kutetea haki za binaadamu na yale ya kijamii kuhusiana na misururu ya visa vya mauaji na ukosefu wa usalama vinavyoshuhudiwa kwa sasa katika mji wa bandari wa Mombasa nchini Kenya.

Mara kadhaa mafisa wa polisi wamekuwa wakilaumiwa kwa kufanya mauaji ya kiholela au kusabisha kutoweka kwa vijana mjini humo katika mazingira ya kutatanisha, lakini sasa baadhi ya mashirika hayo yana mtazamo tofauti kuhusiana na jukumu la jeshi hilo kwenye visa hivi. Kipi kilichobadili muelekeo huu wa maoni ya wanaharakati wa haki za binaadamu kwa polisi? 

Haya yote yanafuatia mauaji ya hivi punde kabisa ya kijana mmoja aliyepigwa risasi na polisi, huku mwanakamati wa usalama katika kijiji kimoja akikatwa mapanga na genge la majambazi. Hali hii sasa imezua mjadala kuhusu hali ya usalama, huku baadhi ya mashirika hayo yakiunga mkono juhudi za jeshi la polisi katika kupambana na magenge ya vijana wanaowahangaisha wakaazi wa mji huu.

Viongozi wa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, Francis Auma kutoka shirika la MUHURI na mwenzake Khalid Hussein kutoka shirika la Haki Africa, wamelaani vikali mauaji ya hivi punde kabisa ya vijana mjini Mombasa. Hivi ni baadhi tu ya visa vya mauaji vinavyodaiwa kufanywa na maafisa polisi dhidi ya vijana wa mitaa ya Mombasa.

Ukosefu wa usalama sasa limekuwa jambo la kawaida katika mji huu wa Mombasa na viunga vyake, huku makundi ya vijana wanaojihami kwa silaha butu wakiendelea kuwashambulia wenyeji ambao sasa wameingiwa na hofu hasa nyakati za usiku.

Mpasuko waibuka kati ya makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusu mauaji ya vijana yanayodaiwa kufanywa na polisi.
Mpasuko waibuka kati ya makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusu mauaji ya vijana yanayodaiwa kufanywa na polisi.Picha: picture-alliance/dpa

Mauaji kadhaa kwa njia ya kutatanisha 

Vijana wasiopungua sita wameuawa na polisi ndani ya muda wa wiki mbili zilizopita na kisa cha hivi punde kabisa kikiwa kile cha kuuawa kwa kijana aliyepigwa risasi Jumatano asubuhi. Wengine waliouawa wiki iliyopita ni pamoja na Bilal Masoudi, kijana wa darasa la tano, Kenga Ramadhani umri wa miaka 19 na Juma Kitsao miaka 19.

Kawaida, maafisa wa polisi ndio wamekuwa wakilaumiwa kwa mauaji ya kiholela au kutoweka kwa vijana mjini Mombasa, ingawa jeshi hilo linasema vijana hao ni wafuasi wa magenge sugu yanayoendelea kuwahangaisha wakaazi wa Mombasa na kuvuruga amani.

Kwa muda mrefu, wakaazi wa mji huu wa bandari wamekuwa wakilifumbia macho suala hili na kuwaachia maafisa wa kutoka mashirika ya kutetea haki za binadamu, lakini sasa kuna muamko mpya unaoyakosoa mashirika haya ya kutetea haki za kibinadamu.

hali hii sasa imezua mgawanyiko miongoni mwa mashirika ya kibinadamu baadhi yao yakidai kwamba hatua zinazochukuliwa na mashirika ya Muhuri na Haki Africa, zinakusudia tu kuyabembeleza magenge hayo na kuzidisha ukosefu wa amani na usalama mjini Mombasa.

Hata hivyo, akijibu kauli hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Binadamu la Haki Africa, Khalid Hussein, alisema kuwa hatua yao hailengi kuwatetea wanachama wa magenge ya ujambazi bali haki kwa wote.

Hali hii ya ukosefu wa usalama katika mji huu wa bandari ambao pia ni kituo muhimu cha shughuli za utalii unatishia kusambaratisha ukuaji wa uchumi kwa kuwaogofywa waekezaji.

Mwandishi: Eric Ponda/DW Mombasa
Mhariri: Mohammed Khelef