Maua yako ya waridi yanatoka wapi?
Kenya ni moja kati ya nchi zinazoongoza katika kuuza maua nchi za nje. Lakini ili kuyakuza maua hayo yanayopendeza na kuvutia kuna athari katika mazingira.
Rangi zinazong’aa na zinazopendeza
Nyumba zilizoko karibu na ziwa Naivasha zinapendeza kama yalivyo mamilioni ya maua yanayopandwa eneo hilo kila mwaka. Likiwa linajulikana kama "kitovu cha maua ya Afrika", eneo hilo lililoko kaskazini ya mji mkuu Nairobi huuza mawaridi na maua mengine ya aina nyinginezo duniani kote. Sekta hiyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi. Lakini kuna madhara yake pia.
Eneo bora na muafaka
Kenya ni nambari nne miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika kuuza maua nchi za nje. Ardhi yenye rotuba, jua la kutosha na maji mengi, hulifanya eneo la ziwa Naivasha kuwa bora na muafaka kwa maua kunawiri. Zaidi ya kampuni 50 za maua zimewekeza katika fuo za Ziwa Naivasha. Kemikali na dawa za kuwadhibiti wadudu huchafua maji. Lakini wafanya biashara wa maua wanasema hawapaswi kulaumiwa.
Maua dhidi ya samaki
Mnamo mwaka 2009, nusura ziwa likauke. Idadi ya samaki ilipungua kwa sababu mara kwa mara kampuni za maua ziliyaelekeza maji ya ziwa kuingia katika mashamba yao na zile nyumba za kuhifadhi maua yaani green houses ufuoni mwa ziwa hilo. Hayo ni kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo. Ilichukua mwaka mzima ndipo idadi ya samaki ilipoanza kuongezeka tena.
Biashara yenye tashwishi
Japo kampuni ziliwekewa masharti magumu baada ya 2009, wavuvi katika ziwa hilo wanawashuku wafanya biashara wa maua ambao wameongezeka katika fukwe za ziwa hilo. Wanaamini kuwa kemikali zinajipenyeza ndani ya maji ziwani. Kampuni zimeyakana madai hayo lakini pia zilikataa kuiruhusu DW kuingia katika nyumba zao za kuotesha maua-greenhouses.
Biashara ya maua isiyochafua mazingira?
DW iliruhusiwa kuzuru shamba la maua la Oserian. Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani GIZ linatoa ushauri kuhusu namna ya kuweza kuendeleza shughuli zake bila kuchafua mazingira. Kampuni ya Oserian inasema hairuhusu maji machafu yaliyotumika kuingia ziwani. Lakini inayatumia tena maji hayo katika nyumba za kuhifadhi maua green houses. Pia ina kitambulisho cha “Biashara iliyo sawa”
Wadudu waitwao 'beetles' wana manufaa
Kampuni hiyo ya maua ambayo imewaajiri takriban watu 6,000, pia imesema inatumia nusu pekee ya dawa zilizokubaliwa kuwadhibiti wadudu na magonjwa. Badala yake wanatumia wadudu waitwao beetle kwa Kiingereza. Kwa mfano katika picha hii mfanyakazi wa Oserian anawaweka 'beetles' kula wadudu wengine waharibifu watakaopatikana kwenye maua hayo ya waridi.
Soko kubwa barani Ulaya
Unapoyazungumzia maua ya mawaridi, yale yanayotoka Kenya ni maarufu sana katika Umoja wa Ulaya ambapo theluthi tatu ya maua hayo hununuliwa. Mengi hununuliwa nchini Ujerumani na Uingereza. Lakini hata nje ya Umoja wa Ulaya, maua kutoka Kenya pia yanapendwa zaidi nchini Marekani na Urusi.