Matumaini yazidi kuwa makubwa nchini Iran | Masuala ya Jamii | DW | 19.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Matumaini yazidi kuwa makubwa nchini Iran

Matumaini ya kiuchumi yameendelea kuwa makubwa Iran kufuatia kuimarika kwa mahusiano kati ya nchi hiyo na mataifa ya magharibi baada ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Kila msafiri anayewasili katika mji mkuu wa Iran, Tehran anakuwa mara moja mteja wa Jeshi la Mapinduzi la Iran. Hii ni kwa sababu wanajeshi wa Jamhuri hiyo ya kiislamu wanaendesha shughuli zao katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini, wakifanya biashara yenye faida kubwa kupitia utozaji wa ada za kuingilia na ndege kutua pekee. Huku wanajeshi hao wakizidhibiti bandari na viwanja vingine vya ndege, Jeshi la Mapinduzi linalojulikana pia kama "Sepah Pasdaran" - linaidhibiti mipaka ya Iran.

Hawalipi ada ya vivuko wala kodi. Huchagua bidhaa zipi waziruhusu kuingia nchini na hawaulizwi ni kiwango gani cha bidhaa hizo zinazoingia katika soko lisilo rasmi - au kiwango gani cha fedha wanachopata kutokana na bidhaa hizi.

Jeshi la Mapinduzi linamiliki ardhi, bahari na vikosi vya wana anga, linadhibiti silaha muhimu za nyuklia na lina jumla ya wanajeshi 120,000. Linaendesha pia biashara kubwa. Linaendesha kliniki zinazotoa matibabu ya magonjwa ya macho. Hujenga mabwawa, kutengeneza magari, barabara kuu, reli na hata njia za chini ya ardhi. Lina mafungamano ya karibu sana na biashara ya mafuta na gesi ya nchi hiyo na linajihusisha pia na uchimbaji madini.

Shughuli za Jeshi la Mapinduzi ni vigumu kuzifahamu na kwa hiyo haziripotiwi sana na vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi.

Biashara katika mavazi ya mashehe

Lakini shughuli za kiuchumi za Iran hazidhibitiwi tu na Jeshi la Mapinduzi. Mashirika ya kidini yanayoongozwa moja kwa moja na mashehe wakuu wa kishia yana ushawishi mkubwa zaidi. Ofisi ya Shirikisho la Ujerumani inakadiria kwamba kampuni za aina hiyo zinadhibiti asilimia hadi 80 ya uchumi wote wa Iran.

Ölförderung in Iran, Öl, Wirtschaft

Jeshi la Mapinduzi limewekeza katika sekta ya mafuta

Hakuna anayefahamu kiwango cha biashara zao. Hazitakiwi kutangaza hadharani mapato yao na hawajawahi kutakiwa watoe maelezo. Wairan wengi waliuliza mabilioni ya dola yalipotelea wapi wakati rais Mahmoud Ahmadinejad alipokuwa madarakani, lakini hawakupata jawabu.

Bahman Nirumand anakumbuka rushwa ilikuwepo chini ya utawala wa kifalme pia lakini hakukuwa na wezi wa kuchomoa vitu mifukoni kama ilivyo kwa wale wenye mamlaka leo.

"Setad" - makao makuu ya mamlaka ya Imam - ni miongoni mwa wakfu za kidini zenye mali ya thamani ya zaidi ya dola bilioni 90. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters, wakfu wa Setad uliasisiwa muda mfupi kabla kifo cha Ayatollah Ruhollah Khomeini, kiongozi wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aliutumia wakfu huo kama nyumba ya kuhakiki mali ya wafuasi wa zamani wa Shah waliopokonywa au kuikimbia nchi, na kuwapa masikini au watu wenye mahitaji. Tangu wakati huo Setad imejengwa kama moja wapo ya kampuni kubwa yenye ushawishi mkubwa, huku ikibakia chini ya kiongozi mkuu wa kidini, Ayatollah.

Nani anayenufaika na kuondolewa vikwazo?

Setad imekuwa chini ya Ayatollah Ali Khamenei tangu mwaka 1989 kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na imewekeza kuanzia katika sekta ya fedha, mafuta na mawasiliano, hadi katika utengezaji wa dawa za kupanga uzazi na kilimo cha mbuni. Matawi mengi ya kampuni ya Setad yalikuwa katika orodha ya hivi ya vikwazo vya Marekani, katika juhudi ya kuyashambulia moja kwa moja masilahi ya kiuchumi ya utawala wa Iran.

Wizara ya fedha ya Marekani inasema Setad si wakfu hatari, lakini ni mtandao wa makampuni unaodhibitiwa na utawala wa Iran kutengeneza na kudhibiti uwekezaji usiorekodiwa katika vitabu, ukifichwa machoni pa Wairan na wakaguzi wa kimataifa.

Kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran na mataifa ya magharibi kwa hiyo kutazinufaisha kampuni hizi zaidi kuliko wananchi wenyewe. Hata hivyo Nirumand ana matumaini kwamba makasha ya fedha ya Iran hayatapungikiwa. "Raia wa kawaida hatapa kitu, kwa sababu biashara itakuwa ikishika kasi zaidi. Na kwa njia hiyo wafanyabiashara na wale wote wanaotoa huduma Iran hawatanufaika kutokana na kuondolewa kwa vikwazo."

Mwandishi: Thomas Kohlmann

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com