Masuali yaulizwa kuhusu mshukiwa wa mauaji Ufaransa
23 Machi 2012Kwa kuwaongezea shinikizo maafisa wa usalama, afisa mmoja wa polisi mkongwe ameuliza jinsi mshukiwa huyo hakuweza kukamatwa akiwa hai wakati wa uvamizi wa jana Alhamisi katika mji wa Kusini Magharibi wa Toulouse. Polisi kutoka kitengo maalum waliingia ndani ya jengo hilo baada ya kulizingira kwa zaidi ya saa 32, na kumuuwa mtu huyo kwa jina la Mohamed Merah aliyedai kuwa ni mwanamgambo wa kundi la al-Qaeda, alipojaribu kufyatua risasi kiholea akitoroka kutoka chumbani mwake.
Tukio hilo lilikuwa limekatiza shughuli za kampeni za uchaguzi wa rais nchini Ufaransa uliopangwa kufanyika Aprili na Mei, lakini Sarkozy alirejelea kampeni yake akitaka kuchaguliwa tena, kwa kuhutubia mkutano wa hadhara mjini Strasbourg jana jioni, ambapo alisema uhalifu huo haukuwa kazi ya mtu mwenye akili punguani. Alisema uhalifu huo ulikuwa ni kazi ya mtu mwenye tabia ya kinyama.
Awali katika taarifa yake iliyorushwa kupitia televisheni, Sarkozy aliapa kuwasaka watu wenye itikadi kali, akisema atawachukulia hatua za kisheria watu wanaozitembelea tovuti za kigaidi au kusafiri hadi mataifa ya ng'ambo kupokea mafunzo ya imani za aina hiyo.
Kampeni za uchaguzi wa rais kuendelea
Kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais kinarejea leo, na masuala yatakayoangaziwa sasa ni ugaidi, usalama, na mtazamo wa itikadi kali nchini humo. Rais Sarkozy atazuru mji wa Kaskazini Valenciennes ambapo anatarajiwa kuikagua miradi ya ukarabati, viwanda, na vyumba vilivyojengwa kwa ajili ya wafanyakazi.
Wanasiasia kadhaa wanauliza jinsi maafisa wa ujasusi wa Ufaransa walishindwa kukomesha msururu wa mauaji yaliyofanywa na Merah ikizingatiwa kuwa alikuwa kwenye orodha ya watu wenye itikadi kali. Mpinzani mkuu wa Sarkozy, Francois Hollande, alisema maswali ni lazima yaulizwe. Kura ya maoni imemwonyesha Sarkozy akiwa mbele ya mpinzani wake Hollande katika duru ya kwanza ya uchaguzi Aprili 22, ijapokuwa ilitabiri Hollande kushinda katika duru ya pili ya Mei 6. Wapiga kura wamemwona Sarkozy kuwa mkweli kuhusu masuala ya usalama na uhamiaji ambayo yanazungumziwa zaidi katika kampeni.
Mshukiwa alikuwa kwenye orodha ya Marekani
Kiongozi mmoja wa ujasusi nchini Marekani alisema mshukiwa huyo alikuwa kwenye orodha ya watu waliopigwa marufuku kusafiri kwa ndege. Orodha hiyo iliundwa na maafisa wa Marekani, inawapiga marufuku wale waliotajwa kusafiri kwa ndege hadi na kutoka nchini humo.
Wakati huo huo Waislamu nchini Ufaransa wanahofia kutengwa kutokana na tukio hilo. Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Front National Party Marine le Pen alikuwa miongoni mwa wale wa kwanza kushutumu itikadi kali za Kiislamu akidai kuwa kila mara amekuwa akionya kuhusu athari zake.
Akizungumza wakati wa kampeni yake jana Le Pen alisema kwa miaka kumi sasa amekuwa akionya kuwa athari ya itikadi kali za kiislamu haitiliwi maanani nchini Ufaransa.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP/IPS
Mhariri: Josephat Charo