1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya kimataifa yaruhusiwa kuzuru jimbo la Rakhine

Isaac Gamba
28 Septemba 2017

Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa wataruhusiwa kuzuru jimbo la Rakhine nchini Myanmar hii leo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza operesheni ya safisha safisha dhidi ya jamiii ya Rohingya walio wachache nchini humo.

https://p.dw.com/p/2krQf
Myanmar Dorf in Rakhine
Picha: DW/A. Rahman Rony

Umoja wa Mataifa umekuwa ukitaka kuzuru eneo hilo tangu mashirika ya kiutu yalipolazimika kuondoka katika jimbo la Rakhine wakati Myanmar ilipoanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya jamii hiyo ya wa Rohingya ambao ni waislamu, mwishoni mwa mwezi Agosti na kusababisha  mamia kwa maelfu kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.

"Kutakuwa na safari iliyoandaliwa na serikali kuzuru jimbo la Rakhine" alisema msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric na kuongeza kuwa ana matumaini kuwa  ni hatua moja wapo katika kuelekea kupata uhuru na urahisi zaidi wa kuzuru jimbo hilo.

Dujarric ameongeza kuwa mkuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa atakuwemo katika ziara hiyo.

Umoja wa Mataifa umeandaa mpango wa dharura kwa ajili ya huduma ya chakula kwa wakimbizi wa Rohingya 700,000.

 Afisa mtendaji mkuu msaidizi wa shirika  la mpango wa chakula duniani Dipayan Bhattacharyya amaesema  hii leo kuwa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yameandaa mpango mpya  kwa ajili ya wakimbizi 700,000 wa jamii ya Rohingya.

Mtendaji Mkuu wa shirika  la Umoja wa Mataifa  linalohusika na masuala ya wakimbizi Fillippo Grandi amesema kwa wale ambao tayari wamekimbilia Bangladesh kurejea kwao kutachukua muda iwapo itatokea na iwapo vurugu zitasimama.

Wahoringya wanakabiliwa na dhiki

Bangladesch, schwangere Rohingya Frau in Flüchtlingscamp
Moja ya changamoto zinazowakabili waisilamu wa Rohongya nchini MyanmarPicha: Imago/T.Chowdhury

Grandi amesema katika majukumu yake, hajawahi kuona watu wenye dhiki kama wakimbizi hawa warohingya.

Jeshi la Myanmar ambalo limekuwa likishutumiwa kuzuia upatikanaji habari kuhusina na operesheni inayoendelea katika mji wa Maungdaw magharibi mwa nchi hiyo hapo jana iliandaa ziara ya vyombo vya habari katika kijiji cha Baw Kyaw ambayo hata hivyo taarifa za hivi punde zinasema zira hiyo imefutwa..

Makaburi makubwa yaliyozikwa miili ya  wanavijiji 45 wa jamii ya Kihindu yaligundulika mapema  wiki hii na jeshi la nchini hiyo linawashutumu wanamgambo kutoka jamii hiyo ya warohingya kwa kuhusika na mauaji hayo.

Hata hivyo kikundi cha uwokozi cha wanamgambo wa Rohingya kimekanusha wanamgambo wake   kuhusika na mauaji hayo pamoja na vitendo vya udhalilishaji kingono au kuwasajli kwa nguvu watu katika jeshi hilo.

Mifupa na miili ya watu waliouawa ilikutwa katika majani katika eneo la  Ye Baw Kyaw huku watu wa jamii ya kihindu waliokimbia eneo hilo wakilieleza shirika la habari la AFP kuwa  washambuliaji waliokuwa wamefunika sura zao walivamia eneo hilo na kuwakatakata baadhi ya watu kwa mapanga na baadaye kuwafukia.

Jeshi la Myanmar limekuwa likijaribu kudhibiti taarifa kuhusiana  na mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kuzuia vyombo vya habari kuzuru eneo lenye mgogoro huku likitoa taarifa za mara kwa mara likiwashutumu wanamgambo wa Rohingya kwa kuhusika na umwagaji damu.

Taarifa za serikali pamoja na jeshi zimekuwa pia zikijaribu kuelezea mateso wanayokabiliwa nayo watu wa jamiii nyingine nchini humo kama vile wabudha walioko katika jimbo la Rakhine na wahindu ambao wameondolewa katika eneo ambalo limekumbwa na machafuko.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/afpe

Mhariri      : Gakuba Daniel