1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya M23 yaua watu 15 mashariki mwa Kongo

5 Machi 2024

Waasi wa M23 inaoaminika wanaungwa mkono na Rwanda wamefanya mfululizo wa mashambulizi kwenye eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo siku ya Jumatatu na kusababisha vifo vya watu 15.

https://p.dw.com/p/4dALB
Mgogoro| M23| Kongo| Rwadwa
Mapigano kati ya M23 na jeshi la Kongo yanawalazimisha maelfu kukimbia maeneo yao mashariki mwa Kongo.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Waakazi, wafanyakazi wa huduma za afya na maafisa wa serikali wamesema mashambulizi hayo yameilenga wilaya ya Rutshuru iliyopo kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini.

Duru zinasema mabomu yalivurumishwa kwenye makaazi ya raia na kusababisha vifo na kuwalazimisha maelfu wengine kukimbia.

Mapigano kati ya M23 na jeshi la Kongo yamepamba moto katika wiki za karibuni hasa kwenye maeneo ya Rutshuru na Masisi.

Hapo jana Jumatatu Umoja wa Ulaya ulijiunga na Marekani pamoja na Ufaransa kuikosoa Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.

Taarifa ya umoja huo imeitaka serikali mjini Kigali kuwaondoa wanajeshi wake ndani ya mipaka ya Kongo  na kusitisha uungaji wake mkono kwa kundi la M23.