1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maseneta wa Marekani kupigia kura azimio la Yemen

13 Desemba 2018

Maseneta nchini Marekani wanatarajiwa kupiga kura juu ya azimio ambalo litaitaka Marekani kuondoa usaidizi wake katika vita vya Yemen, hatua itakayokemea Saudi Arabia baada ya mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi. 

https://p.dw.com/p/3A105
USA Anhörung des Senats zum Atomabkommen mit dem Iran
Maseneta wa chama cha RepublicanPicha: picture alliance/AA/S. Corum

Baraza la seneti pia linaweza kutathmini azimio jingine la kuyalaani mauaji ya Khashoggi wakati maseneta wakitafakari jinsi ya kukabiliana na mauaji ya mwandishi huyo. Maafisa wa ujasusi wa Marekani tayari wameshaamua kwamba Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman alijua kuhusu mpango wa kumuua Khashoggi, lakini Rais Donald Trump amekataa kumlaumu.

Jana Jumatano maseneta 60 walipiga kura kuanzisha mjadala kuhusu azimio la Yemen, kuashiria kwamba walipata uungaji mkono wa kutosha kushinda kura 50 zilizohitajika. Lakini haijabainika jinsi mabadiliko ya hatua hiyo yanavyoweza kuathiri kura ya mwisho ambayo inatarajiwa leo.

Huku idadi ya kutosha ya maseneta wa chama cha Republican wakiwa wanaunga mkono azimio hilo, ambalo liliasisiwa na Seneta wa chama cha Republican Mike Lee wa Jimbo la Utah na Seneta Bernie Sanders wa Vermont, Kiongozi wa Wengi Mitch McConell na WaRepublican wengine wanalipinga.

USA Washington Senator Bob Corker
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Senate la Masuala ya Ushirikiano na Nchi za Kigeni Bob CorkerPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

Maseneta hao walikasirishwa na mauaji ya Khashoggi yaliyotekelezwa mwezi Oktoba mwaka huu pamoja na jibu lilitolewa na Ikulu ya Marekani, na hilo lilisababisha baadhi ya WaRepublican kuunga mkono azimio hilo la Yemen kwa kuwa litaonekana kumkemea mshirika wake wa karibu wa muda mrefu.

Baadhi walikuwa na wasiwasi kuhusu vita nchini Yemen ambavyo mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema vinasababisha raia wengi wao watoto, kushambuliwa kwa mabomu na magonjwa. Mwenyekiti wa Kamati ya baraza la Senate ya Masuala ya ushirikiano na nchi za kigeni Bob Corker ambaye ni Seneta wa chama cha Republican kutoka jimbo la Tenessee, ndiye anayetayarisha azimio jingine la kukemea mauaji ya Khashoggi.

Mkuu wa shirika la Ujasusi la Marekabni CIA, Gina Haspel aliwapa taarifa maseneta kuhusu mauaji ya Khashoggi jana, na Waziri wa Masuala ya Ndani wa Marekani Mike Pompeo na Waziri wa Ulinzi Jim Mattis wanatarajiwa kulihutubia bunge leo. Ikumbukwe Pompeo na Mattis waliwahutubia maseneta mwezi uliopita wa Novemba na kusema hakuna ithibati ya kumhusisha Mohammed bin Salman na mauaji ya Khashoggi yaliyofanyika katika ofisi ya ubalozi mdogo wa Saudi nchini Uturuki.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Josephat Charo