Marekani yasema Rwanda na Kongo zaahidi kupunguza mvutano
8 Novemba 2025
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema katika mkutano mjini Washington, pande hizo mbili "zilitambua kuyumba kwa hatua za makubaliano na kuahidi kuongeza juhudi za kutekeleza Mkataba huo wa Amani wa Washington."
Pande hizo pia zilikubaliana juu ya hatua makhsusi za muda mfupi kuhusu sehemu muhimu za mkataba huo, ikiwa ni pamoja na masharti muhimu ya Rwanda kwamba Kongo ikabiliane na wapiganaji wa kundi la FDLR, lililoundwa na jamii ya Wahutu wanaoaminika kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Taarifa hiyo pia imesema pande hizo mbili zilithibitisha tena kujitolea kwao kujiepusha na vitendo vya uhasama au matamshi, hasa mashambulizi ya kisiasa au lugha ambayo inaweza kudhoofisha au kutatiza utekelezaji kamili wa Mkataba wa Amani.