Marekani yakiri mapambano ya mjini Kobani ni magumu | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yakiri mapambano ya mjini Kobani ni magumu

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema siku ya Jumamosi kuwa mji wa Syria wa Kobani ni tatizo kubwa na gumu, lakini mashambulizi ya angani yamepiga hatua katika kuwarudisha nyuma wapiganaji wa Dola ya Kiislamu.

Vikosi vya wapiganaji wa Kikurdi wanaoulinda mji huo wameutaka muungano unaoogozwa na Marekani kuzidisha mashambulizi ya angani dhidi ya wapiganaji wa IS ambao wamezidi kuuzingira mji huo wa Syria uliyoko mpakani na Uturuki siku ya Jumamosi.

"Tunafanya tunachoweza kupitia mashambulizi ya angani kusaidia kuwarudisha nyuma IS. Kumekuwepo na mafanikio fulani katika eneo hilo," Hagel aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Santiago, mji mkuu wa Chile. "Kiukweli hili ni tatizo kubwa," alisema Hagel akimaanisha Kobani.

Kundi linalofuatalia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria lilisema vikosi vya Wakurd vinakabiliwa na kushindwa kusioepukika mjini Kobani ikiwa Uturuki haitafungua mipaka yake na kuruhusu uingizwaji wa silaha, jambo ambalo serikali mjini Ankara inasita kulifanya.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel.

Kundi kuu la wapiganaji wa Kikurd la YPG lilisema katika taarifa kuwa mashambulizi ya muungano ndani na nje ya Kobani siku nne zilizopita yalisababisha hasara kubwa kwa Dola ya Kiislamu, lakini mashambulizi hayo hayajawa na ufanisi katika siku mbili zilizopita.

Afisa wa kijeshi wa Kikurd, akizungumza na shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kutoka Kobani, alisema mapigano ya mitaani yalikuwa yanafanya iwe vigumu kwa ndege za kivita kuzilenga ngome za wapiganaji wa Dola ya Kiislamu. " Tuna tatizo, ambalo ni vita kati ya kaya," alisema Esmat Al-Sheikh, mkuu wa baraza la ulinzi wa Kobani.

Wakati kundi la IS limeweza kuongeza wapiganaji wake, Wakurd hawajaweza kufanya hivyo. IS imeuzingira mji huo upande wa mashariki, kusini, na magharibi, hii ikimaanisha njia pekee ya uwezekano wa ugavi kwa Wakurd ni mpaka wa Uturuki kwa upande wa Kaskazini.

Shinikizo kwa Uturuki

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria aliitolewa mwito Uturuki siku ya Ijumaa kusaidia kuzuwia mauaji mjini Kobani, akiiomba kuwaruhusu wapiganaji wa kujitolea kuvuka mpaka waende kuwasaidia wapiganaji wa Kikurd wanaoutetea mji huo unaoangaliana moja kwa moja kwa ardhi ya Uturuki.

Uturuki bado haijajibu maombi hayo ya Steffan de Mistura, ambaye alisema anahofia kurudiwa kwa mauaji ya Srebrenica ya mwaka 1995 nchini Bosnia. Viongozi wa Kikurdi nchini Syria wemeiomba serikali ya Ankara kuweka njia kupitia Uturuki, kuruhusu msaada na ugavi wa kijeshi kuufikia mji wa Kobani.

Vifaru vya Uturuki vikifanya doria mpakani Karibu na mji wa Kobani.

Vifaru vya Uturuki vikifanya doria mpakani Karibu na mji wa Kobani.

Mpiganaji wa juu wa Kikurd ameitishia Uturuki kwa uasi mpya wa Wakurd ikiwa itang'ang'ana na sera yake ya kutoingilia kati katika mapambano ya mji wa Kobani.

"Dola ya Kiislamu inapata vifaa kwa wapiganaji, huku Uturuki inaizuwia Kobani kupata silaha. Hata pamoja na upinzani, ikiwa mambo yataendelea hivyo, vikosi vya Wakurd vitakuwa kama gari lisilo na mafuta," alisema Rami Abdul-Rahman, anaeongoza shirika la uangalizi wa haki za binaadamu, linalofutalia mgogoro nchini Syria kwa kutumia vyanzo vilivyoko ndani ya taifa hilo.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alisema siku ya Jumamosi kwamba Jenerali mstaafu John Allen, mjumbe wa Marekani aliepewa jukumu la kuunda muungano wa kimataifa dhidi ya Dola ya Kiislamu, alikuwa ndiyo amerejea mjini Washington na kuripoti kuwepo na maendeleo. "Kuna hatua muhimu zimepigwa na Jenerali Allen, hasa na Uturuki," Hagel alisema mjini Santiago.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre.
Mhariri: Sudi Mnette

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com