1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Marekani kukuza ushirikiano Indo-Pasifiki

Angela Mdungu
14 Desemba 2021

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken, amependekeza mkakati wa kukuza ushirikiano na washirika wake wa bara la Asia kwa kuahidi kuongeza usalama katika eneo la Indo-Pasifiki

https://p.dw.com/p/44ETC
Indonesien Jakarta | Besuch US-Außenminister Antony Blinken
Picha: Olivier Douliery/AFP/Getty Images

Katika ziara yake kwenye mataifa ya Indonesia, Malaysia na Thailand, waziri wa mambo ya kigeni Antony Blinken bila kuitaja China moja kwa moja amelitaja eneo la Indo-Pasifiki kuwa ni kati ya maeneo yanayoendelea zaidi duniani ambapo kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa hayakabiliwi na vitisho au  kushurutishwa. Amesema, Marekani na washirika wake watapambana dhidi ya vitendo vyovyote vinavyokiuka sheria.

Akizungumzia Blinken ameyataja maeneo ya ushirikiano kati ya Marekani na eneo la Indo-Pasifiki kuwa ni masuala yanayohusiana na bahari yakiwemo usalama wa majini, usimamizi wa rasilimali, uhifadhi wa uvuvi , shughuli za kiuchumi, sayansi na teknolojia katika eneo hili ambapo mambo mengi yanatokea katika eneo la bahari na hasa biashara.

Maeneo yatakayotiliwa mkazo katika ushirikiano

Amesema ushirikiano huu unafanyika katika katika kipindi muhimu ambapo mgogoro wa hali ya hewa unatishia bahari, maeno  ya pwani na maisha ya viumbe bahari, hivyo ushirikiano hasa katika masuala ya bahari ni muhimu muhimu kuliko wakati wowote ule.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani ameongeza kuwa Marekani itafanya kazi pamoja na washirika wake ili kulinda utaratibu kulingana na kanuni walizoziunda pamoja kwa miongo mingi ili kuhakikisha kuwa eneo hio linabakia wazi na linafikika. Hata hivyo ameongeza kuwa, madhumuni ya kulinda utaratibu siyo kuiminya nchi nyingine bali ni kulinda haki za mataifa yote ili yaweze kuchagua njia yanayotaka bila vitisho wala kushurutishwa

Indonesien Jakarta | Besuch US-Außenminister Antony Blinken
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony BlinkenPicha: Olivier Douliery/REUTERS

China inadai kuwa karibu eneo lote la Kusini mwa China ni la kwake, licha ya madai hayo kukinzana na  mahakama ya kimataifa na mataifa mengine yaliyo katika maeneo ya Pwani kuwa madai hayo ya China hayana msingi.  Taifa hilo limeukataa msimamo  wa Marekani likisema ni uingiliaji kutoka taifa la nje hatua inayoweza kutishia utulivu wa bara la Asia.

Akijibu kauli ya Blinken, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China Wang Wenbin alipokuwa akizungumza katika mji mkuu wa nchi hiyo amesema Marekani inapaswa kukuza ushirikiano katika eneo badala ya kuweka mipaka katika masuala ya kimtazamo.