Marekani, Umoja wa Ulaya zakosoa hukumu ya kifo dhidi ya Mursi | Matukio ya Afrika | DW | 18.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Marekani, Umoja wa Ulaya zakosoa hukumu ya kifo dhidi ya Mursi

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeelezea wasiwasi kuhusiana na hukumu za kifo zilizotolewa dhidi ya Rais wa Misri aliepinduliwa Mohammed Mursi na watu wengine kadhaa

Mursi alikuwa miongoni mwa zaidi ya washtakiwa 100 waliohukumiwa kifo siku ya Jumamosi kuhusiana na ushirki wao katika tukio la uvunjaji jela ambapo wafungwa walifanikiwa kutoroka wakati wa vuguvugu la mageuzi la mwaka wa 2011.

Marekani imeelezea wasiwasi kuhusiana na hukumu hiyo, ikisema “kila mara inapinga kitendo cha kufanya kesi za watu wengi kwa pamoja na kutoa huku za pamoja. Afisa wa Wizara ya Mambo ya Kigeni amesema “Marekani inaendelea kushinikiza haja ya kuwepo mchakato unaostahili na michakato ya kisheria ya inayomlenga mtu binafsi kwa Wamisri wote kwa ajili ya maslahi ya haki.

Mahusiano kati ya Marekani na Misri yaliporomoka baada ya Mursi kuondolewa madarakani, huku utawala wa rais Barack Obama ukisitisha msaada wa kila mwaka kwa jeshi la Misri wa kiasi cha dola bilioni 1.3. Watalaamu wanasema hukumu hiyo inadhihirisha ahadi ya Sisi kuliangamiza vuguvugu lililodumu kwa miaka 87 la Udugu wa Kiislamu , ambalo lilishinda katika uchaguzi ulioandaliwa baada ya kuanguka Mubarak na ushindi wa urais wa Mursi wa Mei 2012.

Polisi wakiweka ulinzi wakati wa kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa Misri Mohamed Mursi

Polisi wakiweka ulinzi wakati wa kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa Misri Mohamed Mursi

Hukumu hiyo imewasilishwa kwa Mufti Mkuu. Chini ya sheria za Misri, Mufti Mkuu lazima atoe maoni yake kuhusu kama sheria ya kiislamu itaruhusu hukumu ya kifo kwa hatia ya makosa Fulani. Hukumu ya mwisho itatolewa Juni 2. Hukumu hiyo ni ya pili dhidi ya Mursi. Mwezi jana, mahakama hiyo hiyo ilimhukumu kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya kuamuru kukamatwa na kuteswa waandamanaji mwaka wa 2012.

Makundi ya haki za binaadamu yanaishtumu serikali ya Misri kwa kutumia mfumo wa mahakama kuukandamiza upinzani, na hasa chama cha Udugu wa Kiislamu, ambacho kimeorodheshwa kuwa Kundi la kigaidi.

Nao Umoja wa Ulaya umeikosoa hukumu hiyo ukisema ilitokana na kesi iliyokumbwa na dosari nyingi. Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema Misri inastahili kuwahakikishia washtakiwa haki yao ya kushtakiwa kwa njia ya haki na uchunguzi ulio huru. Ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya unaamini kuwa hukumu hiyo itatathminiwa upya baada ya kesi ya rufaa kuwasilishwa.

Mursi Aliongoza kwa mwaka moja tu kabla ya maandamano ya umma yaliyoungwa mkono na aliyekuwa mkuu wa jeshi wakati huo na sasa Rais Abdel Fatah al Sisi kumwondoa madarakani Julai 2013.

Sisi alishinda uchaguzi wa rais Mei 2014 akiungwa mkono na Wamisri waliochoshwa na msukosuko wa kisiasa katika taifa hilo la kiarabu lenye watu wengi, kufuatia vuguvugu la mageuzi la mwaka wa 2011 dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Hosni Mubarak.

Chini ya utawala wa Sisi, mamia ya wafuasi wa Mursi wameuawa, maelfu kufungwa jela na wengine kuhukumiwa kifo baada ya kufanyika kesi za watu wengu kwa pamoja ambazo Umoja wa Mataifa ulisema “hatua hiyo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya karibuni“.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga