1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

CENTCOM: Meli ya misaada ya Gaza imeondoka Marekani

Lilian Mtono
10 Machi 2024

Jeshi la Marekani limesema meli inayopeleka misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza iko njiani baada ya Rais Joe Biden kuahidi kujenga gati ya muda kwa ajili ya kuingiza misaada kwenye eneo hilo lililozingirwa.

https://p.dw.com/p/4dM9l
Mashambulizi katika kijiji cha Al-Ezbah
Mtoto wa Kipalestina akiwa amebeba mfuko wa unga katika nyumba iliyoharibiwa na mashambulizi ya angani ya Israel katika kijiji cha Swedish. Wakazi wengi wa Ukanda wa Gaza wanahitaji misaada kutokana na mzingiro wa jeshi la Israel.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Kamandi Kuu ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, CENTCOM imesema meli hiyo imeondoka Langley-Eustis huko Virginia chini ya masaa 36 tangu Biden alipotangaza nia yake hiyo katika hotuba yake ya Hali ya Taifa siku ya Alhamisi.

Kulingana na taarifa ya CENTCOM, meli hiyo imebeba vifaa vya kwanza vya kujenga gati hiyo ya muda.

Gaza haina miundombinu ya bandari na Marekani inapanga kushirikiana na Cyprus iliyokubali kukagua mizigo, sambamba na maafisa wa Israel na kwa maana hiyo haitakaguliwa tena itakapoingia Gaza.  

Tangazo la Biden linafuatia onyo la Umoja wa Mataifa la kusambaa kwa njaa miongoni mwa Wapalestina milioni 2.3, miezi mitano baada ya Israel kuanzisha mashambulizi kwenye Ukanda huo.