1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali kati ya majenerali hasimu yaendelea Sudan

Admin.WagnerD
2 Mei 2023

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu uwezekano wa kutokea janga la kibinadamu nchini humo ambako mamia kwa maelfu ya watu wamekimbia makwao.

https://p.dw.com/p/4QnHB
WHO yasema mapigano yanaishinikiza sekta ya afya ya Sudan na kuielekeza katika janga
WHO yasema mapigano yanaishinikiza sekta ya afya ya Sudan na kuielekeza katika jangaPicha: AFP

Mkazi mmoja wa Khartoum ameliambia shirika la AFP kwamba hii leo alisikia milio ya risasi ya hapa na pale, mingurumo ya ndege za kivita na makombora ya kuzidungua ndege.

Umwagaji damu umeikumba Sudan tangu Aprili 15 wakati mvutano ulipozuka na kusababisha makabiliano ya risasi kati ya kiongozi mkuu wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake aliyegeuka mpinzani, Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha kijeshi cha Msaada wa Dharura - RSF.

Mamia ya watu wameuawa na maelfu kujeruhiwa huku mashambulizi ya angani na mapigano ya risasi yakishika kasi katika eneo kubwa la Khartoum na kusababisha maelfu ya raia wa Sudan kuhamia nchi jirani. Wengi zaidi hawawezi kumudu safari hiyo ngumu hadi kwenye mipaka ya Sudan, na wamelazimika kujificha ndani ya jiji hilo lenye watu milioni tano,lililokumbwa na uhaba wa chakula, maji na umeme.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba watu zaidi ya laki moja huenda wameyakimbia mapigano na hali ngumu Sudan, ambako milipuko imeutikisa mji mkuu Khartoum kinyume kabisa na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa na majenerali wanaopigana.

Watu laki moja waikimbia Sudan 

Nchi kadhaa tayari zinawaondoa raia wake nchini Sudan
Nchi kadhaa tayari zinawaondoa raia wake nchini SudanPicha: Sgt Paul Oldfield/UK MOD/REUTERS

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikai Wakimbizi - UNHCR Filippo Grandi amesema katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ikiwa mapigano hayatakoma basi watu zaidi huenda wakaikimbia Sudan na kusababisha mgogoro wa wakimbizi.

Afisa wa juu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Abdou Dieng, alionya kwamba hali nchini Sudan huenda ikageuka kuwa janga kamili. Kwa upande wake Rais wa Kenya William Ruto alisema mzozo huo umefikia viwango vya maafa huku majenerali wanaopigana wakikataa kusikiliza wito wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya serikali za nchi za Afrika Mashariki (IGAD), Umoja wa Afrika na jumuiya ya kimataifa wa kusitisha mapigano.

Aidha, Umoja wa Mataifa umesema mahitaji ya misaada ya mwaka 2023 kwa Sudan hayakufikiwa na ni asilimia 14 pekee ya mahitaji hayo yaliofadhiliwa.

Chama cha madaktari nchini Sudan kimesema katika taarifa kwamba kufikia jana Jumatatu raia 436 wameuwawa na wengine 2,174 wamejeruhiwa tangu machafuko yalipozuka Aprili 15. Nchi kadhaa tayari zinawaondoa raia wake nchini Sudan na zingine zikiwemo Urusi na Pakistan zinaendelea na zoezi hilo.

AFPE