1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Machafuko Sudan yatishia kusababisha mgogoro wa kiafya

John Juma
1 Mei 2023

Kufuatia mashambulizi, uporaji na uhaba wa madaktari, hospitali nyingi zimesitisha utoaji huduma za matibabu.

https://p.dw.com/p/4Qkq7
Sudan Angriffe Bombardierung
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Wizara ya afya ya Sudan imesema machafuko yanayoendelea nchini humo yamesababisha vifo vya takriban watu 530, miongoni mwao raia na wanajeshi. Aidha watu 4,500 wamejeruhiwa.

Naye Ahmed al-Mandhari, mkurugenzi wa shirika la Afya Duniani kanda ya mashariki mwa Mediterrania ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba hata kabla ya vita, mfumo wa afya wa Sudan ulikuwa taabani.

Mapigano mapya Sudan, UN yatahadharisha hali mbaya ya kiutu

Na sasa kufuatia mashambulizi ya mabomu dhidi ya hospitali, dawa na bidhaa nyingine za matibabu kuporwa huku madaktari wakiikimbia nchi hiyo, kuna tishio la mgogoro mkubwa wa kimatibabu.

Ametahadharisha kuhusu ongezeko la kitisho cha kutokea mripuko wa magonjwa kama kipindupindu, malaria na magonjwa maradhi mengine.

Kulingana na Mandhari, ni hospitali 16 pekee zinazofanya kazi kwa sasa mjini Khartoum na kuna uhaba mkubwa wa madaktari na wataalam wengine.

Miongoni mwa watu waliopo kwenye hatari zaidi ni takriban wagonjwa milioni nne, miongoni mwao wakiwa kina mama waja wazito na Watoto 50,000 wanaokabiliwa na utapia mlo uliokithiri.

WFP: Machafuko ya Sudan yanaweza kusababisha mgogoro wa kikanda

Makumi ya maelfu ya Wasudan wamekimbia Khartoum na miji mingine, na zaidi ya theluthi mbili ya hospitali hasa katika maeneo yanakoshuhudiwa makabiliano makali zimesitisha utoaji huduma.

Majenerali hasimu wakubali kutuma wawakilishi kwa mazungumzo.

Mapigano yao ya kung'ang'ania madaraka yameyaweka Maisha ya mamilioni ya Wasudan katika hatari huku mashambulizi ya risasi, na makombora ardhini na angani yakiendlea.
Mapigano yao ya kung'ang'ania madaraka yameyaweka Maisha ya mamilioni ya Wasudan katika hatari huku mashambulizi ya risasi, na makombora ardhini na angani yakiendlea.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Majenerali wanaopambana nchini Sudan wamekubali kuwatuma wawakilishi wao Arabia kwa mazungumzo. Mazungumzo hayo yanapigiwa upatu kufanyika nchini Saudi Arabia. Hayo yakijiri, tahadhari imetolewa kuwa machafuko hayo yanatishia kuitumbukiza sekta ya afya katika mgogoro mbaya. John Juma na mengi Zaidi.))

Volker Perthes, afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la Habari la Associated press kwamba ikiwa mazungumzo hayo yatafanikiwa, basi yatalenga zaidi makubaliano ya dhati na kuaminika ya usitishaji vita, chini ya waangalizi wa kitaifa na kimataifa. Lakini ameonya kuwa bado kuna changamoto dhidi ya kuanzisha mazungumzo hayo.

Sudan: Makubaliano ya usitishwaji mapigano kufikia tamati

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema changamoto kubwa Zaidi ni kuhakikisha pande zote zinasitisha kabisa makubaliano kila yanapoafikiwa.

Kulingana na Perthes, mazungumzo hayo yanaweza kufanyika Saudi Arabia au Afrika Kusini.

Tatizo la kutoaminiana kati ya pande zinazozozana

Kwenye picha ni baadhi ya wanamgambo wa kikosi chenye nguvu (RSF) kinachoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Kwenye picha ni baadhi ya wanamgambo wa kikosi chenye nguvu (RSF) kinachoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Kila upande unahitaji njia inayopitia ngome ya mwenzake ili kufika eneo la mazungumzo, lakini kutoaminiana kunazusha changamoto nyingine.

Makubaliano kadhaa ya awali ya kusitisha vita yamepunguza machafuko katika maeneo machache tu. Lakini katika maeneo mengine mapambano makali yameshamiri na kuwalazimisha maelfu kuyakimbia makwao, hatua inayoisogeza nchi hiyo kwenye hatari.

Ikiwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili yatafanyika, basi itakuwa ishara ya kwanza ya juhudi za maelewano tangu machafuko yalipoanza Aprili 15.

Abdel Fattah Burhan, mkuu wa jeshi la taifa anayepambana na Mohammed Hamdan Dagalo, mkuu wa kikosi chenye nguvu cha wanamgambo RSF na ambaye zamani alikuwa naibu mkuu wa jeshi la taifa, wanaonekana kuwa tayari kupambana hadi mwisho.

Vyanzo: APE, AFPE