Mapendekezo ya kubadilisha katiba Kenya yazusha mjadala | Matukio ya Afrika | DW | 22.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mapendekezo ya kubadilisha katiba Kenya yazusha mjadala

Hata kabla ya mapendekezo ya Ekuru Aukot kiongozi wa chama cha Thirdways Alliance kuona mwangaza wa jua, wanasiasa tayari wameanza kuchomoa kucha zao, kuyararua mapendekezo hayo.

Mapendekezo ya kubadilisha katiba yanayopigiwa debe na chama cha Thirdways Alliance kwa jina Punguza Mizigo, yanazidi kuibua homa miongoni mwa wanasiasa, wanaosema sasa kuwa watahakikisha wameyapinga yasifaulu. Mapendekezo hayo yaliyoidhinishwa na Tume ya Kusimamia Mipaka na Uchaguzi yanalenga kupunguza gharama ya kuendesha serikali kwa kupunguza idadi ya wajumbe miongoni mwa mapendekezo mengine. 

Hata kabla ya mapendekezo ya Ekuru Aukot kiongozi wa chama cha Thirdways Alliance kuona mwangaza wa jua, wanasiasa tayari wameanza kuchomoa kucha zao, kuyararua mapendekezo hayo. Licha ya mapendekezo yake kuonekana kumtetea mwananchi ambaye amebebeshwa mzigo wa kugharamia maisha ya kifahari ya wajumbe, wajumbe hao wanaapa kuyazima mapendekezo hayo.

Hiyo ni ishara kuwa, Aukot ana kibarua kigumu cha kufikisha na kuwashawishi wajumbe kuyaidhinisha mapendekezo yake yanayolenga kupunguza idadi ya wajumbe kutoka 416 hadi 147 na hata kuondoa nafasi ya waakilishi wa kike kwenye bunge.

Kizingiti cha Aukot kinazidi kuwa kigumu kwani kwenye uchaguzi mkuu uliopita wakili huyo wa masuala ya kikatiba aliyezoa kura elfu 27 wala hakupata mjumbe ama mwakilishi wa chama chake katika majimbo 47. Hata hivyo mapendekezo yake yanaelekea kupata umaarufu, katika taifa ambalo wajumbe hujiongezea mishahara na marupurupu kila wanapotaka.

Kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale

Kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale

Aukot anapendekeza rais kupata mshahara wa shilingi nusu milioni huku wabunge wakipata mshahara wa shilingi laki tatu, lakini kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Adan Duale ameonya kuwa ataongoza wawakilishi wa majimbo kuyapinga mapendekezo hayo.

Tume ya Kusimamia Mipaka na Uchaguzi iliidhinisha sahihi milioni 1.2 ambazo zilikusanywa na kikundi cha Aukot, lakini atahitaji majimbo 24 kati ya 47 kuyaidhinisha mapendekezo hayo kabla ya kupiga hatua nyingine. Wataalam wa masuala ya siasa wanasema kuwa waasisi wa mikakati ya Kujenga Madaraja nchini hawatakubali kushindwa na mikakati ya Aukot.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga wanathibiti majimbo pamoja na maseneta na wabunge. Wao ndio waasisi wa Mikakati ya Kujenga Madaraja ya Kitaifa. Madaraja hayo yanalenga kuzika tofauti za kikabila na kuliunganisha taifa. Mule Musau ambaye ni mratibu wa asasi ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Kenya, ametilia doa sahihi zilizoidhinishwa.

Mapedekezo hayo yanalenga kupunguza gharama ya kuendesha mabunge kutoka shilingi bilioni 40 hadi bilioni tano. Kwa sasa, kamati ya mikakati ya kuunda madaraja ya Kitaifa pia inazunguka kote nchini kukusanya maoni ya wananchi.