Maoni:Ulingo wa moto kutoka Paris hadi Bamako | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni:Ulingo wa moto kutoka Paris hadi Bamako

Utekaji nyara katika hoteli ya Bamako unadhihirisha mapambano dhidi ya ugaidi yanakwenda mbali nje ya miji mikubwa ya Ulaya. "Miungano isiyo ya kawaida itahitajika," anasema Mkuu wa Idara ya Afrika ya DW Claus Stäcker.

"Sheria ya Sunny 16": muda mfupi kabla mauaji ya kihole mjini Bamako jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, lilituma taarifa ya kuchekesha yenye kichwa hiki cha habari kuhusu kozi ya upigaji picha kwa ajili ya maafisa wa habari wa Mali. Siku moja baadaye, hakuna aliyekuwa akicheka. Wanamgambo wenye misimamo mikali ya dini ya kiislamu wametuma tena ishara nzito iliyo wazi kabisa - ishara kwamba wako tayari na wana ari ya kuendelea na kampeni yao bila huruma, na hasa zaidi baada ya athari walizozisababisha mjini Paris. "Mnaonesha ishara za udhaifu na kutokuwa na uhakika," walionekana wakisema. "Ushindi wetu unaongezeka."

Paris, Ankara, Beirut, Sharm el-Sheikh na Bamako, na Yola na Kano eneo la kusini: tukichora msitari kati ya maeneo yaliyokumbwa na mashambulizi ya umwagaji damu, tunafahamu kile ambacho jeshi huita ulingo wa moto. Eneo hilo ambalo si salama, linalotawaliwa na itikadi kali na mizozo, linakaribia kuizunguka Ulaya.

Miaka 24 iliyopita, mwanajeshi wa cheo cha juu wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, Inspekta Jenerali Klaus Naumann, tayari alionya juu ya "ukanda wa mzozo kutoka Afghanistan hadi Morocco". Wakati huo wengi walidhani alikuwa tu ni afisa wa jeshi mwenye mikakati aliyetia chumvi hatari iliyokuwepo. Kauli ya Naumann wakati huo kwamba umwagaji damu si lazima uwe mwiko kwa wanajeshi wa Ujerumani yenyewe ilivunja mwiko.

Kuondoa ukuta wa moto wa Ulaya

Leo ulingo wa moto uko kilomita kadhaa kutoka Ulaya, na eneo ambalo haliruhusiwi kuwa na shughuli za kijeshi kati ya Mali na Libya ni dogo kuliko eneo kubwa lenye mchanga na ukiwa la Sahara linavyotaka tuamini. Mataifa ya magharibi yamefaulu kuwaondoa viongozi wa kiimla, lakini pamoja na viongozi hao yameuondoa ukuta wa moto ulioilinda Ulaya.

Deutsche Welle Claus Stäcker

Claus Stäcker Mkuu wa Idara ya Afrika ya Deutsche Welle

Utekaji wa hoteli ya Radisson Blu, inayoelezwa kuwa mojawapo ya hoteli zinazolindwa vizuri katika mji mkuu wa Mali, Bamako, hasa ulikuwa ukiilenga Ufaransa, ambayo iliiepusha nchi hiyo kutokana na kitisho cha kusambaratika kwa hatua yake ya kuingilia kati kijeshi mwaka 2013 na hivi karibuni ikafaulu kuwaangamiza viongozi kadhaa wa kigaidi.

Lakini shambulizi la Bamako lilielekezwa pia kwa washirika wa Ufaransa na mtindo wa maisha wa nchi za Magharibi. Kama ilivyotokea katika mashambulizi ya mjini Paris, washambuliaji walikuwa wakitoa ujumbe wa msingi, kufuata nadharia ya mauaji makubwa ya kiholela. Na wanajeshi wa Ujerumani - ambao hivi sasa wako Mali kama wakufunzi - wamenasa katika balaa hilo.

Mwenendo unaofanana

Mashambulizi ya Paris yanaonekana yameimarisha ari ya wapiganaji wa jihad kumwaga damu. Hakuna sababu kuamini kwamba aina fulani ya kamandi ya kimataifa ya kundi la Dola la Kiislamu mjini Raqqa nchini Syria unaratibu mashambulizi katika jangwa la Sahara na eneo la Sahel kupitia simu, telegram yaani app ya kutuma ujumbe wa siri kwa haraka au hata michezo ya kompyuta. Masuhuba hawahitaji mawasiliano ya simu kufanya jambo fulani. Tabia zao zinafanana. Hakuna tofauti yoyote wakijiita "The Sentinels" (Al-Murabitoum) "Defenders of the Faith" - "Walinzi wa Imani" (Ansar Dine) au hata Dola la Kiislamu.

Baadhi ya watu wanaamini Vita vya tatu vya Dunia, au hata vita vya kidini vya dunia, tayari vimeanza. Kauli hizi zinaelekea katika mkwamo. Ni muhimu kushirikiana kwa ajili ya ustaarabu, hata pamoja na washirika wasio wa kawaida kama vile China na Urusi. Wapiganaji wa jeshi hili lisilo na uwiano ni vigumu kuwashinda, lakini ni wachache. Washirika wao wanaweza kutambuliwa na kutengwa kwa kutumia jitihada za pamoja.

Kipengee cha kijeshi hakitaepukika na bila shaka kutoka Bamako hadi Berlin. Kama Ujerumani inataka kupunguza shinikizo dhidi ya mshirika wake nchini Ufaransa na Mali, italazimika kutumia sio tu reki, boti na kamera, lakini vikosi vya mapambano pia chini ya kikosi madhubuti cha Umoja wa Mataifa.

Hatimaye damu itamwagika, kama alivyowahi kuonya jenerali Naumann. Kama Afghanistan, kutakuwa na wahanga Wajerumani. Lakini kuna umuhimu wa kuchukua hatua bila uoga ili watu wenye misimamo ya wastani, raia wa kawaida wasipoteze imani - bila kujali imani hiyo nini nini.

Mwandishi:Claus Stäcker

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Sudi Mnette

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com