Maoni ya wahariri juu ya msaada kwa Ugiriki | Magazetini | DW | 28.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya msaada kwa Ugiriki

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya msaada wa fedha uliotolewa kwa Ugiriki na juu ya upinzani mkubwa dhidi ya hatua ya Rais Morsi ya kujirundikia mamlaka.

Rais Mohammed Morsi wa Misri

Rais Mohammed Morsi wa Misri

Maalfu kwa maalfu ya watu wanaandamana mjini Cairo na katika miji mingine ya Misri kumtaka Rais wa nchi hiyo Mohamed Morsi arudi nyuma katika hatua aliyochukua ya kujirundikia mamlaka na hivyo kuweza kupitisha maamuzi yasiyoweza kupingwa hata na mahakama. Gazeti la "Badische Tagblatt" linatoa maoni juu ya maandamano hayo. Mhariri wa gazeti hilo anasema upinzani dhidi ya hatua iliyochukuliwa na Rais Morsi umechelewa.Na huenda ukawa umechelewa sana. Lakini upinzani huo ndio fursa ya mwisho ya kuleta mabadiliko.

Mhariri wa gazeti la "Badische Tagblatt" anaeleza kwamba njia nyingine ya kuleta mabadiliko, ingelikuwa ni kujiingiza kwa wanajeshi ili kuzuia kuletwa utawala wa Udugu wa Kiislamu.Mhariri wa gazeti hilo anaendelea kusema kwamba wanajeshi hawataipeleka Misri kwenye lengo linalodhamiriwa na wanamapinduzi.Na kwa kweli wanajeshi watalirudisha nyuma gurudumu la maendeleo.Hali ilivyo sasa inaonyesha kwamba dunia inapaswa kuwa tayari kuuona mripuko mwingine wa ghadhabu miongoni mwa wananchi.

Jee ni habari njema kwamba Ugiriki itapatiwa msaada mwingine wa fedha na jumuiya ya kimataifa? Habari hizo zilipokelewa baada ya wajumbe wa Umoja wa Ulaya ,Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF na Benki Kuu ya Ulaya kufikia makubaliano. Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker "anatumia lugha ya tamathali kutoa maoni yake juu ya msaada uliotolewa kwa Ugiriki. Anaeleza: "Damu iliyokuwa inavuja imesimamishwa,jeraha limefungwa bandeji, na sasa mgonjwa, yaani Ugiriki amelezwa hospitalini akiwa bado anahitaji matibabu ya lazima.Licha ya msaada uliotolewa na jumuiya ya kimataifa, hakuna kikubwa sana kilichofikiwa.Kilichopatikana ni muda kidogo ili kuweza kuepusha maafa-yaani kufilisika kwa Ugiriki.Madaktari wanasubiri kumfanyia mgonjwa upasuaji.Ugiriki inahitaji kufutiwa deni lake.Kuahirisha siyo kubatilisha.

Wakati mhariri wa "Neue Osnabrücker" anasema njia ya kuifutia Ugiriki deni haiwezi kuepukwa, mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema wale watakaoubeba mzigo mkubwa wanastahili kuambiwa ukweli.Anasema kwamba kilichofikiwa ni mpango wa kuisaidia Ugiriki ambao ni mgumu kueleweka.Malipo makubwa sana, ambayo yanazidi kuongezeka, yanaahirishwa.Wajerumani ambao ndio, watakaobeba mzigo mkubwa katika kuikoa Ugiriki wanastahiki heshima ya kuambiwa ukweli. Sasa isiwe mwiko tena kuzungumzia juu ya kuifutia Ugiriki deni lake.

Mhariri wa gazeti la "Westdeutsche" anaongeza kwa kutahadharisha kwamba ni vizuri kilingo'a jino bovu ili kumaliza maumivu mara moja, kuliko kuendelea kuwa na maumivu yasiokuwa na mwisho.Siyo jambo zuri kunyamaza juu ya athari ziazoweza kutokea. Ikiwa Ugiriki itajitoa kwenye Umoja wa sarafu ya Euro, bara la Ulaya litakumbwa na vurumai za kisiasa na kiuchumi. "Sote tutaathirika,na hasa Wajerumani."

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Abdul-Rahman