Maoni ya wahariri juu ya mashambulio ya mjini Brussels | Magazetini | DW | 23.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya mashambulio ya mjini Brussels

Wahariri wa magazeti karibu yote leo wanatoa maoni juu ya mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika mjini Brusssels .Watu 31 waliuawa na wengine zaidi ya 270 walijeruhiwa.

Polisi wanalinda usalama katika kitongoji cha Molenbeek

Polisi wanalinda usalama katika kitongoji cha Molenbeek

Mhariri wa gazeti la Westfälische Nachrichten anasema pamoja na huzuni,mashambulio ya jana yanasababisha hasira kwa sababu yametokea katika mji unaoruhusu kustawi kwa ngome ya watu wenye itikadi kali ya kidini.

Mhariri huyo anasema ghadhabu hiyo inatokana siyo tu na hali ya kutupiana lawama juu ya mgogoro wa wakimbizi miongoni mwa nchi za Ulaya bali pia kutokana na kushindwa kushirikiana katika kulinda usalama ili kuiteketeza mitandao ya na miundo mbinu ya magaidi.

Gazeti la "Nordwest" linaelezea wasiwasi juu ya kupungua uhuru wa watu kutokana na mashambulio ya kigaidi. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba kila yanapotokea mashambulio ya kigaidi, idara husika zinakaza sukurubu za sheria, na kwa njia hiyo uhuru wa wananchi unazidi kubanwa.

Hakuna mkakati thabiti dhidi ya "Dola la Kiislamu"

Mhariri wa gazeti la "Nordwest" anasikitika kwamba mpaka sasa watu hawajauona mkakati thabiti wa kupambana na magaidi wa "Dola la Kiislamu" Na kuhusu siasa za ndani mhariri huyo anasema wahusika wanavumilia kustawi kwa kitongoji kama kile cha Molenbeek barani Ulaya kote. Ni katika sehemu kama hizo ambamo magaidi wanaogolea kama samaki majini na hivyo kuweza kujibanza.

Mtuhumiwa wa ugaidi akikamatwa Molenbeek

Mtuhumiwa wa ugaidi akikamatwa Molenbeek

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anashtushwa na idadi kubwa ya mitandao ya kigaidi na jinsi magaidi wanavyoweza kujiandaa na kujitandaza katika miji ya Ulaya. Anasema haitakuwa kutakaa tamaa, kusema kuwa, ni vigumu kujihami kwa asilimia Mia dhidi ya magaidi.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anaeleza kuwa miundombinu ya miji ya Ulaya inatoa mianya inayowawezesha magaidi kupenya. Hata hivyo mhariri huyo anashauri kwamba haitakuwa sahihi kusema inapasa kuizoea hali hiyo.

Kutoka Ujerumani ya kati, gazeti la "Mitteldeutsche" linauliza ni kitu gani kinachoweza kumkasirisha mtu hadi ageuke kuwa gaidi?

Aliekuwa mkuu wa idara kuu ya kupambana na uhalifu nchini Ujerumani mnamo miaka ya sabini,Horst Herold, alilijibu swali hilo kwa kueleza kwamba,inapasa mtu ajaribu kuingia ndani ya fikira za adui yake. Katika mazingira ya leo maana yake ni kwambna magaidi wa "Dola la Kiislamu" si maadui wanaotoka nje. Watu hao ni sehemu ya jamii. Wamezaliwa na kukulia katika nchi kama Ubelgiji, Ufaransa , Uingereza na Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche" anasema chuki waliyokuwa nayo, watu hao, haitokei Syria,Lebanon au Irak.

Mashambulio ya jana mjini Brussels yamesababisha madhara lakini pia yameonyesha jinsi watu walivyoshikamana dhidi ya magaidi. Hayo ni maoni ya mhariri wa gazeti la "Volksstimme" Anasema kwa mara nyingine magaidi wameshambulia katikati ya Ulaya.

Mhariri anasema ni vigumu kuhakikisha usalama kwa asilimia mia.Lakini pia anatilia maanani kwamba yumkini magaigi wamevitumia vipenyo vilivyomo katika mfumo wa usalama nchini Ubelgiji. Ndiyo kusema kila upenyo uliopo ni madhara makubwa kwa jamii!

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com