1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Warepublican watumbukia katika mzozo

2 Machi 2016

Hata katika Jumanne Kabambe Donald Trump ameshinda na anaonekana hazuiliki. Je ana fursa ya kushinda dhidi ya Hillary Clinton? Warepublican wanakabiliwa na kitisho cha kutumbukia katika mzozo wa kuaminika.

https://p.dw.com/p/1I5Mi
USA Vorwahlen Präsidentschaftswahlen Super Tuesday Donald Trump
Picha: Reuters/C. Bergin

Kwa mara nyingine tena Donald Trump ameshinda katika majimbo kadhaa katika uchaguzi wa awali wa mchujo jana kuwania uteuzi wa mgombea urais wa chama cha Republican na anaonekana hawezi kuzuiwa, isipokuwa pengine na chama chake mwenyewe, ikiwa kitakataa kuwasikiliza wapiga kura na kuamua kumteua mgombea mwingine tofauti. Hilo lakini haliwezekani katika demokrasia, anasema mwandishi wetu Ines Pohl kutoka mjini Washington, katika maoni yake.

Hillary Clinton ndiye mshindi wa wazi wa chaguzi za Jumanne Kabambe. Ni dhairi sasa kwamba hawezi kuzuiwa, baada ya kushinda wajumbe wengi moja kwa moja na amehakikishiwa kuungwa mkono na wajumbe wengi wanaolezwa kuwa wajumbe kabambe. Licha ya kushinda katika majimbo manne katika hali ya heshima na dhima kubwa, mpinzani wa karibu, Bernie Sanders, hatoi tena kitisho kikubwa kwa Clinton.

Kinachodhihirika wazi dhihiri shahiri ni kwamba historia inaandikwa, na jambo la kusisimua linatokoea. Kuna uwezekano mkubwa sana kwamba Hillary Clinton atakuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kugombea urais nchini Marekani. Amekuwa akipigania kuingia ikulu kwa miaka kadhaa. Hakuna udhalilishaji wala masuala ya mumewe, rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, wala vikwazo vya kisiasa, ambavyo vimemzuia. Mtizamno wake ni kwamba sio tatizo kuanguka kutoka juu ya farasi, tatizo ni kutompanda tena farasi baada ya kuanguka.

Nidhamu na utashi

Hillary Clinton ni kioo cha uadilifu na ari ya kisiasa, lakini haitokuwa haki kusema ana shauku ya kutaka madaraka. Amekuwa akipigania kile anachokiona kuwa ulimwengu ulio bora na wenye haki zaidi. Mpango wa huduma za afya kwa Wamarekani wa rais Barack Obama, maarufu kama ObamaCare, haungefaulu kama si kwa kazi yake kubwa aliyoifanya Clinton.

Pohl Ines Kommentarbild App
Mwandishi wa DW mjini Washington, Ines Pohl

Sio lazima kukubaliana naye katika maoni yake kuhusu siasa na uchumi, lakini ni muhimu kutaja kujitolea kwake kwa dhati sasa. Marekani mwaka huu wa 2016 ni zaidi ya Donald Trump.

Naweza kusema aliyeshindwa sana katika siku ya Jumanne Kabambe ni chama cha Republican. Bilionea Donald Trump alishinda katika majimbo 7 kati ya 11 na sasa anaungwa mkono na wajumbe 258. Kama ilivyotarajiwa, Ted Cruz alishinda katika jimbo la Texas, lakini ushindi wake hafifu jimboni Oklahoma ulikuja kama jambo la kushangaza, na kuifanya idadi ya wajumbe wanaomuunga mkono kuwa 110.

Lakini sasa muujiza unahitajika ili amshinde Trump. Kinyang'anyiro cha kuwania uteuzi wa chama cha Republican kinaonekana kufika ukingoni kwa seneta wa jimbo la Florida, Marco Rubio. Hakuweza kutimiza matumaini ya Warepublican vijana wenye misimamo ya wastani waliyokuwa nayo kwake baada ya maneno yake ya kumshambulia Trump hivi karibuni. Kwa hiyo sasa chama cha Republican kinaingia katika awamu tete.

Mgombea wao wenyewe?

Je wajumbe wa Republican wanatakiwa kweli kumteua Trump kama mgombea wao urais katika mkutano mkuu wa chama msimu wa kiangazi? Baadhi ya Warepublican mashuhuri wameanza kuzungumzia waziwazi juu ya kukataa kumuunga mkono Trump, na kuhusu kutafuta mgombea mwingine. Lakini ni ujumbe upi kuhusu demokrasia ambao hatua hii itauotoa kwa wapiga kura katika majimbo binafsi? Licha ya wasiwasi wa chama cha Republican, wajumbe wanaotilia maanani na kuthamini sana chaguzi watalazimika kuyakubali matokeo.

Pamoja na hayo, Donald Trump amewahi kutangaza kuwa angegombea kama mgombea huru ikihitajika. Bila kuungwa mkono pengine, lakini kwa ushahidi kwamba hazuiliki. Hata na chama ambacho amejiingiza kwa niaba yake katika kampeni na ambacho huenda kikatumbukia katika mzozo wa kuendelea kuaminika kama kitamgeuka. Ni mfano wa mtanziko usiowakabili tu miungu wa Ugiriki bali ulimwengu mzima.

Mwandishi:Pohl, Ines (DW Washington)

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman