Maoni: Ulaya na Marekani zashindwa kutimiza wajibu wake kwa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maoni: Ulaya na Marekani zashindwa kutimiza wajibu wake kwa Syria

Rais wa Syria Bashar al-Assad amekuwa madarakani kwa miaka 20 sasa. Hili limewezeshwa kwa sehemu kubwa na msaada kutoka Urusi na Iran, lakini pia kwa sababu mataifa ya Magharibi yameiacha Syria katika shida.

Syrien, Damaskus: Bashar al-Assad im Interview mit der Britischen Mail on Sunday

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Hayo ni maoni ya mwandishi wa DW Rainer Sollich anayeangazia miaka 20 ya utawala wa rais Assad na taifa lake lililotumbukia katika janga kubwa.

Kwa mtazamo wake, Bashar al-Assad anaweza kujivunia miaka yake 20 madarakani mpaka sasa. Ameweza kuusambaratisha uasi wa kudai demokrasia uliozuka mwaka 2011- na shukran kwa msaada mkubwa kabisa wa kijeshi kutoka Urusi na Iran, ameshinda kimsingi kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuatia uasi huo.

Wapinzani wake, ambao sasa wamebakia makundi machache tu ya wapiganaji wa Kiislamu, wanadhibiti maeneo madogo ya nchi.

Zaidi ya hapo, mataifa ya Magharibi yaliona kwamba kwa kulinganishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS), na makundi mengi ya kigaidi, yalioonesha matendo yao ya kikatili katika mtindo wa kipekee, yeye ni shetani mwenye nafuu.

Shinikizo la Assad kujiuzulu limepungua 

Sollich Rainer Kommentarbild App

Mwandishi wa DW, Sollich Rainer

Serikali za mataifa ya Magharibi na waangalizi wameacha kutoa wito wa kumtaka ajiuzulu. Na ingawa upinzani wa kidemokrasia ulipata wahurumiaji wengi barani Ulaya na Marekani mwanzoni, upinzani huo sasa umesahauliwa. Assad anaweza kulihesabu hili pia kuwa moja ya mafanikio yake.

Rais wa Marekani Donald Trump anaonekana kushughulikia mambo yake ya ndani na ameanza kuonyesha dalili za kujiondoa hatua kwa hatua katika mzozo wa eneo hilo japo wakati mwengine hubadili misimamo yake.

Mtangulizi wa Trump Barack Obama alikuwa tayari ameonyesha jinsi sera ya Magharibi ya Syria ilikuwa ya ujinga wakati hakufanya hivyo kwa tishio lake la kuingilia kijeshi ikiwa serikali ya Assad itavuka "mstari" na kutumia silaha za kemikali.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umezingatia zaidi kupeleka misaada ya kibinadamu nchini humo na inafanya kila iwezalo kuzuia wakimbizi kutoka Syria kuingia Ulaya.

Bado hakuna matumaini nchini Syria

Umoja wa Ulaya umekubaliana na Uturuki, ambayo sasa imekuwa kama mlinzi katika mlango wa kuingia Ulaya. Kwa sasa kila mtu anatazama kimya kimya jinsi hali inavyoendelea hasa katika kambi za wakimbizi Ugiriki. Hakika, mataifa ya magharibi yamewatelekeza raia wa Syria.

Hata hivyo, bado kuna matumaini kuwa raia wa Syria waliodhulumiwa huenda wakapata haki baada ya kesi kuanzishwa katika Umoja wa Ulaya dhidi ya raia wa Syria wanaoshukiwa kuhusika na uhalifu wa kivita nchini humo. Kama ilivyo kwa makundi ya wapiganaji, wafuasi wa Assad pia watabebeshwa dhamana kwa makosa waliyoyafanya.

Ni muhimu kwa kesi za watu binafsi kuchunguzwa na iwapo watapatikana na hatia, basi sheria ichukue mkondo wake. Tunatumai kuwa ipo siku ambayo kutaanzishwa uchunguzi huru wa kutambua jukumu la mataifa ya ghuba na Uturuki kwa kuyafadhili makundi ya wapiganaji.

Ikiwa kweli kutakuwepo na haki nchini Syria, basi mtuhumiwa mkuu atapatikana katika Ikulu mjini Damascus na washirika wake wakiwa Moscow na Tehran.

Mwandishi: Babu Abdalla

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com