Maoni: Ugaidi kitisho kikuu karne ya 21 | NRS-Import | DW | 17.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Maoni: Ugaidi kitisho kikuu karne ya 21

Mashambulizi ya kinyama dhidi ya skuli inayoendeshwa na jeshi huko Peshawar, yaliyouwa zaidi ya watu 140 yanathibitisha kwamba ugaidi hauna macho na kama yanavyosema maoni ya Florian Weigan.

Waombolezaji wakibeba jeneza la mmoja wa wanafunzi waliouawa na Taliban mjini Peshawar, Pakistan.

Waombolezaji wakibeba jeneza la mmoja wa wanafunzi waliouawa na Taliban mjini Peshawar, Pakistan.

Ni wazi kwamba hata mataifa ya kihafidhina ya Kiislamu kama ilivyo Pakistan hayawezi kukwepa kitisho cha siasa kali za kidini. Hata wale wanaoripoti kutoka maeneo ya migogoro, watakuwa lazima wamefadhaishwa mno na kiwango hiki kikubwa cha ukatili. Na kwa hakika hilo ndilo lililokuwa lengo kuu la washambuliaji.

Kwa kuilenga skuli na kuuwa mamia watoto 137 na walimu wao tisa, kundi la Taliban nchini Pakistan lilifanikiwa kuvuta kiwango kikubwa cha makini za kilimwengu. Kuilenga taasisi inayoongozwa kijeshi ilikuwa hatua ya makusudi na kwa kitendo chao hicho, Taliban ilitaka kupiga kwenye kiini cha jamii ya Pakistan.

Lakini wacha tuwe wawazi: skuli hizi zinazoongozwa na jeshi nchini Pakistan si vyuo vya mafunzo ya kijeshi. Watoto wa maafisa wa kijeshi na pia wa raia wa kawaida, zaidi kutoka tabaka la wenye nacho, huenda kwenye taasisi hizi kusaka elimu kwani ni miongoni mwa skuli bora kabisa nchini humo. Kwa kuishambulia skuli hii, Taliban wamelipiza kisasi chao cha kikatili kwa jeshi la Pakistan na pia maafisa wa serikali mjini Islamabad.

Taliban bado ina nguvu

Florian Weigand wa Idhaa ya Pashtun ya DW.

Florian Weigand wa Idhaa ya Pashtun ya DW.

Kwa miezi kadhaa sasa, jeshi la taifa hilo la Asia ya Kusini limekuwa likiendesha operesheni dhidi ya wanamgambo hao kwenye mkoa wa kaskazini magharibi unaopakana na Afghanistan. Mara kadhaa, majenerali wa kijeshi wamejisifia mafanikio ya mashambulizi yao, lakini kwa ukweli hawajaweza kuwamaliza magaidi hao. Kutokana na operesheni hiyo, maelfu ya raia waliojikuta wakinasa katikati ya mapigano kati ya jeshi la wanamgambo wamekimbia makaazi yao.

Kwa jeshi la Pakistan, kuna sababu zaidi sasa za kuiandama Taliban. Makundi hayo ya wanamgambo yaliwahi huko zamani kuwa na lengo moja tu kuu, nalo ni kuiangusha serikali ya Afghanistan na kupambana dhidi ya wanajeshi wa kigeni mjini Kabul huku wakituhumiwa kupata msaada kutoka Islamabad. Lakini mara tu serikali ya Pakistan ilipowageuka, wanamgambo kadhaa wakaungana pamoja dhidi ya serikali hiyo.

Kilichofuatia ni mduara wa papo kwa papo wa mashambulizi na mashambulizi ya kupambana na mashambulizi hayo, na hadi sasa hakuna njia rahisi ya kuumaliza mduara huo. Wakati vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO vikijitayarisha kuondoka Afghanistan siku chache zijazo, Pakistan inapaswa kujifunza somo moja muhimu: yeyote anayeumiliki mkoa wa Hindu Kush, ugaidi hautamalizika. Madhali watu wa maeneo ya mbali ya Pakistan hawana fursa ya ajira na maendeleo ya kiuchumi, Taliban wataendelea kuwavutia wapiganaji wapya kwa ahadi za maisha mema peponi.

Ugaidi ni kitisho kikubwa kabisa cha dunia kwenye karne hii ya 21, na hata kwenye mataifa ya kihafidhina ya kidini kama Pakistan, hakuna njia ya kuuepuka.

Mwandishi: Florian Weigand
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com